Mkazi wa Kijiji cha Lyapona, Kata ya Kaengesa, Sumbawanga mkoani Rukwa, Victoria Kalungwizi (67), ameuawa kwa marungu kwa tuhuma za kuiba mahindi shambani.
Tukio hilo lilitokea juzi katika kijiji hicho saa 11 jioni kwa Kalungwizi kupigwa na watu katika sehemu mbalimbali za mwili kwa fimbo na rungu hadi kufariki dunia. Kutokana na tukio hilo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Rukwa, George Kyando, alisema Jeshi la Polisi mkoani hapa linawasaka watu watatu wanaodaiwa kumuua mtu huyo.
Alisema chanzo cha mauaji hayo ni tuhuma dhidi ya Kalungwizi kuwa mwizi wa mahindi. Alisema alishukiwa kuwa ameiba mahindi katika shamba la Michael Mkombozi. Kamanda Kyando alisema mbinu waliyotumia watu hao ni kumvizia akiwa anavuna mahindi katika shamba ambalo si lake.
Alisema baada ya kumkuta walianza kumshambulia kwa kumpiga sehemu mbalimbali za mwili kwa fimbo na marungu hadi kumsababishia kifo papo hapo. Kamanda Kyando alisema baada ya watuhumiwa kutekeleza mauaji hayo, walitoroka na kukimbilia kusikojulikana na kwamba juhudi za polisi kuwatafuta zinaendelea.
Kyando aliwataka wananchi kuacha kujichukulia sheria mikononi kwa kuwaua watuhumiwa bali wawe wanawafikisha kwenye vyombo vya sheria ili sheria ichukue mkondo wake.
HT @ Nipashe
from Blogger http://ift.tt/2t3dd2z
via IFTTT