UAMUZI WA BODI YA MIKOPO KWA WALIOSITISHA MASOMO AU KUKUTWA NA VYETI FEKI

Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) imesema kuwa, haijalishi mnufaika wa mkopo wa elimu ya juu alipatwa na kadhia ya vyeti feki au alifeli shule na hivyo kusitishiwa masomo, ilimradi alikopa anatakiwa kulipa deni lake.
Akizungumza Dar es Salaam jana na waandishi wa habari, Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB, Abdurazack Badru alisema, hadi sasa tayari wamekusanya Tsh 216.9 bilioni kati ya Tshh 427.7 bilioni za mikopo iliyoiva ambayo ipo tayari kukusanywa. Pia imesema licha ya kuendelea kuwatafuta wadaiwa sugu 100,000 kwa sasa, katika mwaka wa 2016/17 walifanikiwa kuvuka lengo la makusanyo waliyojiwekea ambapo walikusanya bilioni 116 kutoka lengo walilojiwekea la bilioni 76.
Badru alisema kuwa mafanikio hayo yametokana na hatua tatu kuu za kuhakikisha marejesho ya mikopo yanafanyika, ambazo ni pamoja na kuwatafuta wadaiwa sugu wa kuanzia mwaka fedha 1994/95.
Alitaja hatua nyingine mbali na kutoa ankara kwa wadaiwa kuwa ni kuwatafuta wanufaika, kupata taarifa zao muhimu pamoja na ukaguzi mahali pa kazi. Kwa mujibu wa Badru, hadi kufikia Juni mwaka huu, wanufaika 139,259 walitambuliwa na kuanza kulipa marejesho ya mikopo yao.
Miongoni mwa wanufaikaji wengi waliochangia kiasi hicho cha fedha wapo katika sekta ya umma ambao wamewekewa mfumo mrahisi wa kuwabaini na kurejesha mikopo hiyo, alisema Badru.
“Sekta binafsi nayo imetusaidia ingawa kundi la waliojiajiri mfano kuendesha bodaboda na wanaoendesha kilimo na ujasiriamali mwingine lenye wanufaika 28,893 nalo limerejesha jumla ya Sh bilioni 13.7 na kutuonesha mwitikio mkubwa zaidi,” alieleza.
Akielezea miongoni mwa changamoto ambazo wanakumbana nazo sana alisema ni kutokuwa na taarifa za baadhi ya wanufaikaji sehemu wanapofanyia kazi kama wameajiriwa au kujiajiri, lakini pia baadhi ya waajiri ama kwa makusudi au kutokuju hawawasilishi michango ya wafanyakazi wao wanayowakata.
Badru alisema wamewafikisha mahakamani waajiri watatu ambao ni kampuni kwa makosa hayo ya kukaa na fedha za marejesho ya mikopo ilhali wamekwishayatoa kwenye mishahara ya wanufaika ambao ni waajiriwa wao.
ASANTE KWA KUTEMBELEA MTANDAO WETU!!

from Blogger http://ift.tt/2tdZZLr
via IFTTT