TFF Wakanusha Kutowalipa Posho Serengeti Boys

Kufuatia taarifa zilizokuwa zikienea na kusambazwa kwenye mitandao ya kijamii, zikidai kuwa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limewatelekeza wachezaji wa timu ya mpira wa miguu ya Tanzania ya vijana wenye umri wa chini ya miaka 17(Serengeti Boys), TFF imejitokeza na kukanusha taarifa hizo.
Taarifa hizo za uongo zilidai kuwa Serengeti Boys hawakulipwa posho na kushutumu viongozi wa juu wa shirikisho kuhusu jambo hilo.
“Tunapenda kuwajulisha wazazi na umma kwa ujumla kwamba vijana wetu walilipwa posho zao zote wakiwa kambini Morocco na Cameroon na zile za mashindano ya AFCON nchini Gabon.” wamesema TFF
Kwa mujibu wa Taarifa kutoka TFF, zimeeleza kuwa Shirikisho linafanya taratibu za kupeleka maombi kwenye Mfuko wa Maendeleo ya Mpira wa Miguu (Football Development Fund FDF) ili kuweza kuwalipa vijana na benchi la ufundi sehemu ya posho zilizokuwa bado hazijakamilishwa wakati wa michuano ya kufuzu kwa AFCON 2017.
“Tumeshtushwa na taarifa hizo ambazo tafsiri yake ni kuharibu uhusiano mwema kati ya shirikisho, wazazi na wachezaji ambao wanatarajiwa kuitumikia timu ya Taifa ya Vijana wenye umri wa chini ya miaka 20 maarufu kama Ngorongoro Heroes.”
TFF wamesema kuwa wanawatambua vijana wa Serengeti Boys kwani bado ni sehemu ya kikosi cha Ngorongoro Heroes na hivyo ukifika wakati wataitwa kambini kwa ajili ya michezo ya kimataifa ya U-20.
Aidha, Wametoa shukrani kwa kuushukuru umma ambao wameendelea kuchangia Mfuko wa FDF ambao kimsingi kazi yake ni kutafuta rasilimali kwa ajili ya maendeleo ya mpira.
“Tunaomba michango iendelee kwani bado tuna changamoto za mashindano mbalimbali kwa timu za wanawake na vijana ikiwemo fainali za wanawake Afrika zitakazofanyika Ghana hapo mwakani kwa timu ya Twiga Stars na AFCON 2019 kwa Serengeti Boys ambayo itakuwa mwenyeji.”
Mfuko wa Maendeleo ya Mpira – FDF ulianzishwa kwa lengo la kutafuta rasilimali za maendeleo ya mpira wa miguu hasa kwa wanawake na vijana pamoja na miundombinu ya mchezo huo.
ASANTE KWA KUTEMBELEA MTANDAO WETU!!

from Blogger http://ift.tt/2rfbtCe
via IFTTT