MKUU wa Wilaya ya Bagamoyo, Majid Mwanga, amewapiga marufuku askari mgambo wilayani hapa wanaokamata pikipiki zinazobeba abiria, maarufu kama bodaboda na kuonya kuwa hiyo si kazi yao.
Mwanga alitoa onyo hilo juzi alipokuwa katika ziara ya kusikiliza kero mbalimbali zikiwamo za maji na umeme zinazowakabili wananchi wa Kata ya Lugoba, Halmashauri ya Chalinze.
Alhaji Mwanga alisema hayo baada ya kupokea malalamiko kutoka kwa wananchi kuhusiana na vitendo vya mgambo kukamata bodaboda.
Alisema mgambo ambao ni askari wa akiba. Hivyo hawaruhusiwi kukamata bodaboda kutokana na kwamba si askari waliopewa jukumu hilo.
“Askari mgambo ambao ni askari wetu wa akiba hamruhusiwi kukamata bodaboda kwani si askari mliopewa jukumu hilo. Kwa kufanya hivyo mnakwenda kinyume cha sheria, ” alisema Mwanga.
Naye Mkurugenzi wa Kituo cha Uzalishaji Maji katika Mto Wami, Mhandisi Christina Mchomba, akizungumzia kero ya maji, alisema utafiti walioufanya katika mto huo umebaini uwapo wa tope kubwa.
Kutokana na kero hiyo, alisema wanaendelea na mradi huo kwa kufanya upanuzi wa mitambo ambayo inaenda sambamba na ujenzi wa matangi 19 ambayo yatasaidia kuhifadhi maji.
Mchomba alisema moja ya matangi hayo linajengwa katika kijiji cha Mazizi lenye uwezo wa kuhifadhi lita milioni mbili, litasaidia kero ya muda mrefu ya upatikanaji wa maji katika kijiji hicho.
from Blogger http://ift.tt/2rk1pDh
via IFTTT