TAARIFA MPYA KUHUSU KESI YA VIGOGO WA ESCROW NA MALI ZAO

Serikali imekamata mali za wafanyabiashara Harbinder Singh Sethi na mwenzake James Rugemalira wanaohusishwa na uchotwaji wa zaidi ya Sh bilioni 300 katika Akaunti ya Tegeta Escrow.
Mali hizo zimekamatwa siku chache baada ya Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Tanzania (Takukuru) kuwafikisha watuhumiwa hao mahakamani.
Kwa mujibu wa gazeti la MTANZANIA Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), Biswalo Mganga hakuweza kupatikana kutoa ufafanuzi wa kina wa hatua ya ofisi yake kushikilia mali za Sethi na Rugemalira.
Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), iliiambia MTANZANIA jana kuwa Serikali imelazimika kukamata mali zote za wafanyabiashara hao kama hatua ya kuzuia kuuzwa au kuhamishwa umiliki wake wakati wakiendelea kusota rumande.
“Ni jambo la kawaida katika kesi kama hii, huwezi kuacha mali ambazo ndizo kielelezo katika suala hili. Hivyo hatua ya kwanza ni kumkamata mshtakiwa na kisha ni lazima udhibiti mali zake kwani ndiyo kielelezo muhimu kinachobishaniwa katika kesi husika.
“Unaweza ukaiacha mali halafu mshtakiwa huku akiwa yupo ndani bado akaendelea kutoa maelezo na mali kuhamishwa umiliki wake au hata kuuzwa, kwa hali hiyo ndiyo hulazimika kushikilia mali hizo,” alisema mtoa taarifa huyo ambaye hakupenda kutajwa jina lake .
Ofisi ya DPP inaelezwa imezuia mali zote za Sethi na Rugemalira kwa kuziweka chini ya ulinzi mkali pamoja na kufunga kwa muda akaunti zao za benki.
Sethi ambaye ni Mwenyekiti Mtendaji wa Kampuni ya Independent Power Tanzania Limited (IPTL)/Pan Africa Power (PAP) na Rugemalira wa Kampuni ya VIP Engineering and Marketing Ltd, walifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam Juni 19.
Watuhumiwa hawa tayari wamesomewa mashtaka sita, yakiwamo ya uhujumu uchumi.
Mbali na hayo imeelezwa kuwa orodha ya waliopata mgawo wa fedha hizo za Escrow imezidi kuongezeka, wakiwamo vigogo kutoka wizara nyeti, taasisi, viongozi wa dini na mashirika yasiyo ya kiserikali na tayari baadhi yao wameanza kuhojiwa na Takukuru mapema wiki hii.
Taarifa za ndani zinaeleza kuwa idadi ya waliohojiwa imefika zaidi ya watu 30 hadi sasa.
Miongoni mwa wanaotajwa kuhojiwa na Takukuru wamo baadhi ya mawaziri wa Serikali ya Awamu ya Nne na mtoto wa kigogo wa Serikali, ambao inaelezwa kuwa huenda wakafikishwa mahakamani Jumatatu, huku wengine wakiendelea kuhojiwa zaidi.
ASANTE KWA KUTEMBELEA MTANDAO WETU!!

from Blogger http://ift.tt/2t91PBw
via IFTTT