ONYO LA SERIKALI KWA WANAOMPINGA RAIS KUHUSU MIMBA KWA WANAFUNZI

WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwigulu Nchemba ametishia kuzifutia usajili asasi zisizo za kiserikali (NGOs) ambazo zimeendelea kusisitiza na kudai haki ya mwanafunzi wa kike aliyejifungua kurudi shule na pia zile zinazohamamisha mapenzi ya jinsi moja nchini.
Nchemba amesema kuwa, anaunga mkono kauli ya Rais John Magufuli ya wanafunzi kutoruhusiwa kurudi shule kwa kwa asilimia 100 na kwamba asasi hizo za kiraia zinazoendelea kutetea mambo hayo, hatosita kuzifutia usajili.
Akizungumza wakati wa harambee ya kuchangia ujenzi wa Kanisa Katoliki la Bikira Maria Mama wa Yesu, Parokia ya Kisasa Mjini Dodoma jana, Mwigulu Nchemba alisema kuwa suala la mimba za utotoni/wanafunzi na mapenzi ya jinsia moja, ni mambo yanayokwenda kinyume na tamaduni zetu kama watanzania na kwamba yeye kama kiongozi hawezi kuyafumbia macho.
Nchemba ambaye alikuwa kanisani hapo kwa niaba ya Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alisema kuwa asasi hizo zinazojificha kwenye kivuli cha haki, zitafute kazi nyingine ya kufanya.
Aidha, alishangaa baaadhi ya watu ambao ni waumini wa dini kulifanya jambo hilo la mimba kwa wanafunzi kuwa la mjadala, huku akiwauliza huwa wanatumia Biblia gani inayoruhusu masuala hayo.
“Kwa imani yangu, maandiko yote ninayopitia, kwanza yanazuia mimba nje ya ndoa, na yote yanazuia mimba za utotoni. Kwa hiyo mimi namuunga mkono Mhe Rais kwa asilimia zote,” alisema Nchemba.
Nchemba alisema yeye ambaye ni mteule wa Rais, agizo hilo lililotolewa si suala la kujadiliwa kwani ndio msimamo wa serikali, na yeye kazi yake ni kutekeleza.
“Aliyosema Rais ni maagizo na si ajenda ya mjadala, na kwenye hilo hatukusanyi ushauri wala maoni, huo ndio msimamo wa serikali, hakuna ushoga, hakuna mimba kwa wanafunzi.”
Mbali ya asasi hizo, Nchemba aliwaonya pia wananchi ambao ni raia wa Tanzania kuwa wakibainika kujihusisha na mapenzi ya jinsia moja watafikishwa kwenye vyombo vya sheria huku akisema wale ambao si raia watafukuzwa nchini.
Nchemba alisema kuwa wale wote wanaotaka wanafunzi wenye mimba na waliojifungua kurejea shule, wakafungue shule zao lakini kwa shule za serikali, hilo haliwezekani.
Waziri huyo aliwasihi Watanzania kuendele kumuombea Rais Magufuli azidi kutekeleza ahadi zake kwani hayo anayoyafanya ni kwa faida za watanzania wote.
“Akijenga reli, sio kwamba ataihamishia kwake, au amejenga mabweni basi atapangisha, ila haya anayafanya kwa maslahi kwa faida ya Watanzania,” aliongeza.
ASANTE KWA KUTEMBELEA MTANDAO WETU!!

from Blogger http://ift.tt/2tML9Nn
via IFTTT