Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana na Mwenyekiti wa Tume hiyo, Jaji Damian Lubuva, wapigakura hao wanatakiwa kutambua kuwa mpigakura atakayekuwa na kadi ya kupigia kura ila namba ya kadi ni tofauti na namba iliyopo kwenye daftari la kituoni, ataruhusiwa kupiga kura.
Alisema aidha wapigakura ambao picha zao hazionekani vizuri au hazionekani kabisa kwenye Daftari la Kudumu la Wapigakura, wapigakura hao wataruhusiwa kupigakura. Lubuva pia alisema wapigakura walioandikishwa na tume na wanaishi katika maeneo mapya ya kiutawala, yaliyogawanywa wakati au baada ya kujiandikisha, hivyo majina ya maeneo hayo kutofautiana na majina yaliyopo kwenye kadi zao, wataruhusiwa kupiga kura.
Alisema wapigakura ambao hawaonekani kwenye mfumo wa daftari, lakini wana vitambulisho vilivyotolewa na tume na fomu zao za kuandikishwa kufikishwa Tume na majina yao kuandaliwa katika mfumo wa orodha, bila picha na kupelekwa katika vituo walivyojiandikisha, wataruhusiwa kupigakura.
“Kwa mujibu wa sheria, mpigakura ni lazima awe na kadi ndio aruhusiwe kupigakura. Hivyo, mpigakura asiye na kadi hataruhusiwa kupiga kura,” alisema Lubuva. Alisema wapigakura ambao wana kadi ya kupigia kura, lakini hawamo katika Daftari la Kudumu la Wapigakura kituoni, hawataruhusiwa kupigakura.
Kesi ya kukaa mita 200 vituoni Katika hatua nyingine, kesi ya kikatiba kuhusu uhalali wa kukaa mita 200 kutoka kituo cha kupiga kura, inatarajiwa kusikilizwa leo katika Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam.
Kesi hiyo iliyofunguliwa na Mgombea wa Viti Maalum (Chadema) Jimbo la Kilombero mkoani Morogoro, Amy Kibatala inatarajiwa kusikilizwa mbele ya jopo la majaji, Sekieti Kihiyo, Lugano Mwandambo na Aloycius Mujulizi.
Amy kupitia wakili wake, Peter Kibatala, amefungua kesi hiyo chini ya hati ya dharura dhidi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) na Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC).
Anaiomba mahakama itoe tafsiri ya Kifungu cha 104 (1) cha Sheria ya Uchaguzi Sura ya 343 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2010, kama kinazuia wananchi kukaa kwa utulivu mita 200 baada ya kupiga kura katika vituo vyao.
Aidha, anaiomba mahakama iseme na kutafsiri kifungu hicho, kinamaanisha nini kuhusu haki ya wapiga kura. Kesi hiyo imefunguliwa kutokana na kauli iliyotolewa na NEC kwamba wananchi wakishapiga kura, hawaruhusiwi kukaa eneo la vituo vya kupigia kura umbali wa mita 200.
Aidha, inaitaka mahakama itamke kama ni halali kwa NEC kuzuia wananchi kukaa kwa utulivu umbali huo au la, pia iseme kuwa kauli ya kuzuia haki ya wananchi ni uvunjifu wa Katiba ya nchi.
HABARI LEO