Helikopta iliyomuua Filikunjombe ni ya Kalonzo


HELIKOPTA iliyoanguka na kusababisha vifo vya watu wanne akiwamo mgombea ubunge wa jimbo la Ludewa kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Deo Filikunjombe na rubani wake, Kapteni William Silaa, ilikuwa mali ya Makamu wa Rais wa zamani wa Kenya, Kalonzo Musyoka.

Kwa mujibu wa mtandao wa The Star wa Kenya, helikopta hiyo AS 350B3 Eurocopter yenye namba za usajili 5Y-DKK5Y-DKK na iliyokuwa na namba ya uzalishaji 7027, ilikuwa imekodiwa na mgombea huyo kwa ajili ya kampeni zake jimboni Ludewa mkoani Njombe.

Mbali na Filikunjombe, wengine waliopoteza maisha katika ajali hiyo iliyotokea Alhamisi iliyopita baada ya helikopta hiyo kuanguka kwenye pori la Selous wilayani Kilombero mkoani Morogoro ni Casablanca Haule na Egid Nkwera waliokuwa wakitoka Dar es Salaam kwenda Njombe.

Helikopta hiyo ilikuwa na uwezo wa kubeba mzigo usiozidi tani moja na kuruka urefu wa futi 20,000 kutoka ardhini. Wachunguzi wa ajali za ndege nchini Tanzania, wamechukua baadhi ya vitu kutoka katika mabaki ya helikopta hiyo iliyoteketea kwa moto ili kuchunguza chanzo cha ajali hiyo.

Helikopta hiyo ni moja ya helikopta nyingi zilizosajiliwa nchini Kenya ambazo zimekodiwa na wagombea mbalimbali wa urais na ubunge kwa ajili ya kampeni za uchaguzi zinazoendelea.

Kalonzo alinunua helikopta hiyo ya kisasa kwa ajili ya kampeni za uchaguzi mkuu wa mwaka 2013 na imekuwa ikikodiwa ndani na nje ya Kenya kwa shughuli mbalimbali.

HABARI LEO