Na Mwandishi Wetu
KIFO cha Mchungaji Christopher Mtikila (65) aliyezaliwa mwaka 1950, kimezua utata ambapo baadhi ya watu wa karibu na mwanasiasa huyo wanadai kwamba ‘ameuawa’.
Akizungumza kwa sharti la kutotajwa jina lake gazetini, mmoja wa watu hao amesema licha ya Jeshi la Polisi nchini kusema kwamba kifo hicho kilichotokana na ajali iliyosababishwa na mwendo kasi, lakini kuna kila dalili za ‘mkono wa mtu’ kutokana na harakati za mwanasiasa huyo katika masuala ya kijamii, kitaifa na kimataifa.
Mchungaji Mtikila, Mwenyekiti wa Chama cha DP na kiongozi wa kanisa la Full Salvation, alifariki dunia katika ajali ya gari iliyotokea usiku wa kuamkia jana Jumapili Oktoba 4, 2015 katika Kijiji cha Msolwa mkoani Pwani wakati akitokea Morogoro.
“Hatuwezi kuridhika kwamba ni ajali tu, lakini tunaliomba Jeshi la Polisi lifanye uchunguzi wa kina kuhusiana na kifo hicho, kwani kuna mashaka makubwa kwamba huenda ameuawa kabla ya ajali hiyo kutokea kutokana na mambo ambayo Mchungaji alikuwa akiyafuatilia kwa muda mrefu,” alisema mtu huyo wa karibu na Mtikila.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Jaffar Mohammed, amelieleza Ijumaa Wikienda kwamba, ajali hiyo ilitokea majira ya saa 11:45 alfajiri ambapo gari hilo aina ya Toyota Corolla Namba T 189 AGM lilikuwa likiendeshwa na George Steven ‘Ponera’ (31), mkazi wa Mbezi, Dar ambapo chanzo chake ni mwendo kasi uliosababisha gari kuacha njia na kupinduka.
Chanzo chetu cha habari kinaeleza kwamba, kauli za hivi karibuni za Mchungaji Mtikila kuhusu masuala ya ufisadi kwa baadhi ya wagombea urais nchini Tanzania pamoja na siasa za kimataifa zinazohusisha mataifa jirani nazo zinaweza kuwa chanzo na akaonya kwamba uchunguzi wake usiishie kujua chanzo cha ajali ya gari.
Hata hivyo, kutokana na utata huo, tayari dereva wa gari hilo, George Ponera anashikiliwa na polisi kwa mahojiano zaidi.
Chanzo: Global publishers.co.tz