CHADEMA Wazidi Kuikaba Koo Tume Ya Uchaguzi......Wasema Watatangaza Matokeo Ya Urais Kabla Ya Tume Kuyatangaza



TUME ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imebanwa mbavu ikitakiwa kutoa hadharani Daftari la Kudumu la Wapiga Kura kwa mujibu wa uandikishaji wa wapigakura ulivyofanyika nchi nzima.

Sambamba na kibano hicho mbele ya waandishi wa habari jana, Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kilirudia msimamo wake wakuyatangaza matokeo ya urais kabla ya Tume hiyo kwa kuwa kura zinahesabiwa vituoni na matokeo kubandikwa kabla ya kuwasilishwa kituo kikuu cha tume kwa ajili ya majumuisho.

Naibu Katibu Mkuu wa CHADEMA, John Mnyika alisema kwamba chama hicho ambacho safari hii kinashirikiana na vyama vingine vitatu chini ya muungano wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) kimeshaamua kutozembea kwa namna yoyote ile kuhusu matokeo ya uchaguzi mwaka huu.

“Mabere Marando alishasema kuwa mwaka huu tutatangaza wenyewe matokeo kabla ya Tume kwa kuyajumlisha kutoka katika vituo vya kupigia kura nchi nzima, msimamo wetu bado ni hai tutatangaza wenyewe hata kama watasema ni uchochezi,” amesema.

Marando ambaye ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema na wakili maarufu wa Mahakama Kuu nchini, alitoa kauli hiyo iliyonukuliwa na gazeti la MAWIO, wakati akielezea maandalizi ya UKAWA katika kudhibiti uchakachuaji wa matokeo.

Kwa mujibu wa sheria za Tanzania, hakuna haki ya kuhoji matokeo ya urais wakati wa uchaguzi mkuu. Haki hii imekuwa moja ya madai ya vyama vya upinzani nchini kwa muda mrefu.

Mnyika ambaye alikuwa mbunge wa Ubungo, safari hii akigombea jimbo jipya la Kibamba lililochomolewa ndani ya Ubungo, alitoa uzoefu wa jimboni kwake ambako mwaka 2010, alitangaza matokeo ya kura zake kabla ya Tume baada ya kuona mpango wa kumuibia ushindi wake.

“Kutangaza matokeo kabla ya tume ndio jambo lililonisaidia kutoporwa ushindi wangu 2010. Kile kilichotuokoa Loyola (eneo la kutangazia matokeo ya Ubungo) ni sisi kutangaza matokeo kwa wananchi na kuishinikiza tume iyatangaze pia,” alisema.

Msimamo huo unasisitizwa na CHADEMA wakati tayari Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Jaji mstaafu Damian Lubuva ameshasema watatangaza matokeo ya urais ndani ya siku tatu (saa 72) na utaratibu utakuwa kura kuhesabiwa kituoni, matokeo yake kubandikwa kituoni na nakala itaskaniwa na kupelekwa kituo kikuu cha Tume.

“Hakutakuwa na wizi wa kura katika uchaguzi wa mwaka huu. Hao wenye wasiwasi kwamba kura zao zitaibiwa kama wanajua mianya ya wizi wa kura waje walete taarifa na tume itatumia mamlaka yake kuzima mianya yote, si kwa zege tu bali hata kwa kutumia nondo,”alisema Jaji Lubuva.

Jaji Lubuva amekuwa akisema kwamba safari hii kumewekwa utaratibu wa kiteknolojia usiotia shaka wa kuzidhibiti kura dhidi ya uwezekano wa kuchakachuliwa na kwamba wamedhamiria kutangaza matokeo vituoni hata ya urais ili kuondoa hofu na kuwawezesha wananchi kurudi kwenye shughuli za ujenzi wa taifa.

Mnyika katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika eneo la Ngome ambako ndiko makao makuu ya UKAWA kwa ajili ya uchaguzi, alisema wakati umefika Tume itoe orodha ya wapigakura na kujiandaa kuondoa hitilafu zitakazobainika.

“NEC imetangaza jana wapiga kura wote ni milioni 23.7 lakini maelezo yao wanadai idadi kamili itafahamika kadri muda na uhakiki unavyoendelea. Huu ni mkanganyiko, tunatoa wito watoe rasmi orodha ya wapiga kura kwa vyama vya siasa,” alisema.

Alisema panahitajika kuundwa tume shirikishi inayohusisha vyama vyote ambayo itakagua orodha ya wapiga kura na kuona kama kuna utata wowote ili utatuliwe.

Mnyika alieleza kuwa uandikishaji kwa mfumo mpya wa kielektroniki (BVR) na hata uhakiki wa majina umetawaliwa na utata na “inaonekana tayari tume inalo daftari lake ambalo vyama kama wadau wa kwanza wa uchaguzi huo hawana mpaka sasa.”

Tume imetangaza kwamba uchaguzi huu utakuwa na vituo 72,000 natayari vifaa vya uchaguzi vimewasili nchini, zikiwemo karatasi za mfano huku Jaji Lubuva akisema karatasi halisi zitaletwa nchini wiki moja kabla ya Oktoba 25 na kudhibitiwa na Tume yenyewe kwa ajili ya usalama.
Mpekuzi blog