Jengo la madarasa wanayotumia wanafunzi wa darasa la pili na la tatu kutokana na upungufu wa vyumba vya madarasa katika shule hiyo.
Na.Jumbe Ismailly
[Ikungi, Singida]Shule ya msingi Taru namba saba iliyopo kata ya Sambaru, tarafa na wilaya ya Ikungi, Mkoani Singida haijasajiliwa kwa kipindi cha miaka sita sasa, hali inayochangia wanafunzi wa darasa la nne kutembea umbali wa kilomita 22 kwenda kufanya mtihani wa kuingia darasa la dano katika shule mama ya Sambaru.
Mwenyekiti wa Kijiji cha Sambaru, Mfaume Hassani Masudi aliyasema hayo baada ya kutakiwa na mtandao huu kutoa maelezo ya sababu zipi zilizochangia shule hiyo kutosajiliwa licha ya kuwa na wanafunzi 200 wa darasa la awali hadi darasa la tano lakini mpaka sasa bado haijasajiliwa.
Alifafanua mwenyekiti huyo kwamba shule hiyo inayoingia mwaka wa sita sasa ina vyumba vya madarasa matatu, nyumba moja ya mwalimu na matundu ya vyoo imeshindikana kupata usajili kutokana na uongozi uliopita wa serikali ya Kijiji hicho kutopeleka taarifa sahihi za kuwepo kwa shule hiyo wilayani.
“Kwa hiyo tatizo lililokuwepo ni kutokana na shule yetu hii ya Taru namba saba kama inavyojulikana ni shule ambayo imeanza na sasa hivi inaingia mwaka wa sita,wanafunzi wapo lakini shule bado haijasajiliwa huku ikiwa na vyumba vya madarasa matatu na nyumba moja ya mwalimu”alifafanua.
“Lakini tatizo ambalo tumeendelea kulifuatilia baada ya sisi kuingia kwenye madaraka ndiyo hilo ambavyo tulivyosema kwamba taarifa tumeambiwa hazijapelekwa kule wilayani kwamba kuna shule inatakiwa isajiliwe”alibainisha mwenyekiti huyo wa kijiji.
Hata hivyo Masudi alisisitiza kwamba baada ya kubaini hilo utaratibu uliofanywa na ofisi yake ni kuandaa muhtasari wa serikali ya Kijiji hicho wanaotarajia kuupeleka kwenye kikao cha kamati ya maendeleo ya kata hiyo (WDC),kikao ambacho hakijaitishwa na ofisa mtendaji wa kata hiyo tangu walipochaguliwa.
Kwa mujibu wa mwenyekiti huyo inavyoonekana shule hiyo ilianzishwa kwa mazingira ya kisiasa baada ya wazazi kuamua kujenga shule hiyo ambayo mbunge wa jimbo hilo, Tundu Lissu ndiye aliyekuwa akitoa misaada mbalimbali katika shule hiyo ikiwemo kuwalipa posho walimu wanaofundisha wanafunzi wa shule hiyo.
“Kwa sababu shule ilianza kisiasa,wazazi waliamua wajenge shule pale kwa hiyo na msaada ukaonekana unatolewa na mbunge sasa viongozi waliokuwepo wa serikali ya Kijiji walikuwa wanatokana na CCM,na kwa kuwa mbunge huyo ni wa CHADEMA hivyo hawakuona umuhimu wa kuisajili shule hiyo”alisisitiza mwenyekiti huyo.
Kwa upande wake ofisa mtendaji wa Kijiji cha Sambaru,Baraka Njiku licha ya kukiri kwamba alishiriki kuanzishwa kwa shule hiyo kuanzia mwanzo mpaka sasa na walipokutana na uongozi wa kata na kujiridhisha kukamilika kwa taratibu zinazotakiwa kusajiliwa ndipo walipowaita wakaguzi kwenda kukugua vyumba vya madarasa na nyumba ya mwalimu na kukubaliwa kuomba usajili wa shule hiyo.
“Baada ya wakaguzi kukagua vyumba vya madarasa matatu, nyumba ya mwalimu pamoja na matundu ya vyoo baadaye wakasema kwa hatua mliyofikia mnaweza mkaomba shule isajiliwe,tulifanya hivyo,tulipewa idadi ya wanafunzi waliopo pale shuleni maagizo ambayo aliyapeleka ofisi za mkurugenzi mtendaji wa wilaya ya Ikungi”aliweka bayana mtendaji huyo.
Hata hivyo Njiku hakusita kuwatahadharisha viongozi wa chama na serikali kuacha kuweka kipaumbele masuala ya itikadi za kisiasa kwenye masuala ya maendeleo ili shule hiyo iweze kufanikiwa kupatiwa usajili kwani mwakani wanafunzi hao haifahamiki watafanya mtihani wa kuingia darasa la sita katika shule gani.
Naye mwenyekiti wa shule ya msingi Sambaru,Senge Jumanne alisema katika moja ya vikao vyao walivyokutana na mratibu wa elimu kata ya Sambaru walielezwa masharti ya kusajili shule hiyo kuwa na vyumba vitatu vya madarasa,nyumba za walimu pamoja na matundu ya vyoo,masharti ambayo tayari yamekamilishwa na wananchi wa Kitongoji hicho.
Alipotakiwa kuzungumzia sababu za shule hiyo kutosajiliwa kwa kipindi kirefu,mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Ikungi,Mohamedi Nkya licha ya kukiri kutosajiliwa kwa shule hiyo,lakini alisema amemwagiza ofisa elimu wa wilaya hiyo kulishughulikia suala hilo haraka iwezekanavyo kabla ya mwezi jan,mwaka ujao ili shule hiyo iwe imesajiliwa kupunguza usumbufu kwa wanfunzi kutembea umbali mrefu kufuata elimu.
Moja ya aina ya madawati wanayotumia wanafunzi hao wanaotarajiwa kupikwa tayari kwa ajili ya kuanza darasa la kwanza hadi kuendelea masomo ya madarasa ya juu katika shule hiyo ya Taru namba saba.
Moja ya darasa linalotumiwa na wanafunzi wa darasa la awali na darasa la kwanza katika shule ya msingi Taru namba saba kwa ajili ya kuandaliwa kuendelea na masomo ya madarasa ya juu zaidi.
Ni sehemu inayotumiwa na wanafunzi wa darasa la nne katika shule ya msingi Taru namba saba kutokana na upungufu wa vyumba vya madarasa uliopo katika shule hiyo.
Ni moja ya darasa linalotumiwa na wanafaunzi wa madarasa mawili huku likiwa na madawati machache ikilinganishwa na wanafunzi waliopo katika darasa hilo.
Ni ratiba ya masomo ya kuanzia darasa la kwanza hadi la nne katika shule ya msingi Taru namba saba,ikiwepo ukutani licha ya shule hiyo kuwa na upungufu mkubwa wa vifaa vya kufundishia na kujifunzia.
Ni ubao unaotumika kuandikia masomo mbalimbali kwa wanafunzi wa madarasa ya pili na tatu uliotafunwa na mchwa kutokana na idara ya elimu katika Halmashauri ya wilaya ya Ikungi kutoitambua shule hiyo na kuipa kipaumbele katika ugawaji wa vifaa.
Ni choo kinachotumiwa na wanafunzi pamoja na walimu wa shule ya msingi Taru namba saba,hali inayochangiwa kwa namna moja au nyingine baadhi ya wanafunzi kwenda kujisaidia vichakani wanapozidiwa.Picha zote na Jumbe Ismailly