Na Stephano Mango, Mbinga.
MAGARI mawili yaliyokuwa katika msafara wa kampeni wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika kijiji cha Mtua, kata ya Mpepai wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma yameharibiwa vibaya baada ya watu wanaodaiwa kuwa ni wafuasi wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kuvamia msafara huo, na kurusha mawe huku watu waliokuwemo ndani ya magari hayo nao wakinusurika kuumia vibaya.
Tukio hilo lilitokea Septemba 19 mwaka huu majira ya jioni, ambapo Katibu wa CCM wilaya ya Mbinga, Zainabu Chinowa ndiye aliyekuwa akiongoza msafara wa kampeni wa chama hicho katika kata ya Mpepai na vijiji vyake kwa lengo la kumnadi mgombea wa nafasi ya udiwani kupitia tiketi ya chama hicho, Benedict Ngwenya.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi, Chinowa alisema kuwa wakati wakiwa barabarani wanarudi wakitokea katika kijiji cha Mtua ghafla waliona magogo makubwa ya miti yakiwa yamewekwa barabarani, ili kuzuia wasiweze kupita na baadaye walipojaribu kuyatoa ndipo kundi la vijana lilijitokeza na kuanza kuwarushia mawe, ambayo yaliweza kuharibu na kuvunja vioo vya magari hayo yaliyokuwa katika msafara huo.
“Kwa kweli tumenusurika kuumizwa vibaya, gari letu la chama limevunjwa kioo cha ubavuni na gari lingine moja ambalo ni la mgombea wetu nalo limevunjwa vunjwa karibu vioo vyote, tumeripoti Polisi ili hatua ziweze kuchukuliwa”, alisema Chinowa.
Chinowa alieleza kuwa waliohusika katika tukio hilo, ni wafuasi wa CHADEMA ambapo wakati wanafanya unyama huo, wengine walionekana wakiwa wamevalia sare za chama hicho.
Mwandishi wa gazeti hili ameshuhudia magari hayo yakiwa kituo cha Polisi wilaya ya Mbinga, ambapo gari la CCM wilaya lenye namba za usajili T 545 BEW aina ya Landcruiser Hardtop limevunjwa kioo cha ubavuni upande wa kushoto na lingine aina ya Landrover Discover, lenye namba T 797 AEN nalo limevunnjwa vunjwa vioo kwa mawe hayo ambayo yalikuwa yakirushwa.
Kaimu Kamanda wa Polisi wa mkoa wa Ruvuma, Revocatus Malimi alipohojiwa na waandishi wa habari alisema kuwa taarifa kamili bado hazijamfikia ofisini kwake na kwamba, anaendelea kufanya mawasiliano na Mkuu wa Polisi wilaya ya Mbinga ili aweze kupata undani wa tukio hilo.