DK.SLAA ATANGAZA RASMI KUACHANA NA SIASA



Aliyekuwa Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo CHADEMA, Dk. Wilbroad Slaa akizungumza na waandishi wa habari katika hoteli ya Serena jijini Dar es Salaam leo.
 
Baadhi ya wananchi pamoja na waandishi wa habari wa vyombo mbalimbali vya habari wakimsikiliza aliyekuwa Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo Dk.  Wilbroard Slaa leo katika hoteli ya Serena jijini Dar es Salaam.


Aliyekuwa Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo Dk. Wilbroad Slaa amesema leo kuwa amejiondoa kwenye siasa na hatajiunga na chama kingine chochote cha siasa ila ataendelea kuwatumikia Watanzania kwa namna yoyote.
Dk Slaa amesema alichukua uamuzi huo tangu Julai mwaka huu baada ya kutofautiana na chama chake juu ya masharti ya kumpokea mgombea wa urais kupitia Chadema chini ya mwavuli wa Ukawa, Edward Lowassa.
Dk. Slaa akizungumza jijini Dar es Salaam leo, amekiri kushiriki vikao kujadili ujio wa waziri mkuu huyo wa zamani lakini alishangazwa na viongozi waandamizi wa chama chake kuharakisha kumpokeea pasipo kutimiza masharti aliyopendekeza.
“Sina tabia ya kuyumbishwa….sina chuki na mtu yoyote lakini sipendi siasa za udanganyifu na propaganda,” amesema Dk. Slaa na kusema ameachana na siasa tangu 28 Julai, 2015 baada ya kuona misingi ya chama alichoshiriki kukijenga imepotoshwa.
Sharti la kwanza ambalo Dk. Slaa alitaka lizingatiwe ni kiongozi huyo wa zamani ndani ya serikali ya CCM kujisafisha kwenye tuhuma ya kashfa ya Richmond aliyohusishwa nayo akiwa kama Waziri Mkuu.
Aidha, Slaa alitaka ajue Lowassa ataongeza thamani gani ndani ya Chadema, ikiwa ni pamoja na viongozi watakaojiunga toka chama tawala.
Baada ya Lowassa kutokidhi vigezo tajwa, huku akiwataja viongozi waliojiunga Chadema wakitokea CCM wakiwa ni “mizigo” ndani ya chama tawala, amejiweka kando na Chadema.
DK Slaa ametumia takribani saa mbili kueleza msimamo wake na matatizo anayoyaona kwa Lowassa na waziri mkuu mstaafu ambaye naye amejiunga na upinzani, Frederick Sumaye kuwa hawafai na si watu safi.