Dhana 5 potofu kuhusu Muungano wa Tanganyika na Zanzibar


 Serikali tatu ni neema ya vyeo kwa wanasiasa

I. KATIKA mfumo wa serikali tatu,  gharama zitakuwa zaidi ya trilioni tatu zinazosemwa na Jaji Joseph Warioba, kwa kuwa hatutaweza kukwepa gharama mpya za kiuendeshaji za Serikali ya Muungano inayojitegemea kama vile majengo, watumishi vitendea kazi na mengineyo.Ongezeko hilo maana yake ni kodi na michango zaidi kutoka nchi washirika. Serikali tatu ni neema kwa wanasiasa, kwa sababu itapanua vyeo lakini msiba kwa wananchi watakaolazimika kuigharimia kwa kodi zaidi.


    Takwimu zilizoainishwa katika makala yangu ya kwanza katika gazeti lililopita zinashindwa kunishawishi kuwa mantiki ya serikali mbili kama ilivyokubaliwa na
waasisi wetu imepitwa na wakati. Sioni ni kwa vipi, muundo wa serikali tatu leo hii utalinda utaifa wa Zanzibar dhidi ya hofu ya kumezwa huku ikipunguza gharama za uendeshaji wa Muungano wenyewe.Utaifa wa Tanganyika haujatoweka kutokana na ukubwa wake na tishio la Uzanzibar kutoweka bado upo ikiwa tutakuwa na serikali moja kama takwimu za idadi ya watu zinavyoonyesha.


    Ikiwa kweli tunayo dhamira ya kuendelea na Muungano, basi njia yenye uhalisia ni serikali mbili sio tatu wala moja. Mazingira yaliyosababisha kuwapo kwa serikali mbili yangali hayajabadilika hata sasa.Ni kweli muundo wa serikali mbili una changamoto zake, lakini changamoto hizo zinatokana na mfumo zaidi kuliko muundo na tunaweza kurekebisha mfumo ndani ya muundo uliopo.


    Changamoto za muundo wa serikali mbili zinahimilika kuliko changamoto za serikali tatu au moja zitakazoibua changamoto za gharama na utaifa wa Uzanzibari. Hivyo, nachelea kusema dhana kwamba tatizo ni muundo wa serikali mbili na kwamba serikali tatu ni suluhisho ni dhana potofu. Haya ni maelezo ya dhana ya kwanza, niliyoanza kuichambua katika makala yangu toleo lililopita la gazeti hili. Dhana ya pili ni Zanzibar kunyonywa, Tanganyika kufaidi zaidi.

    II. Tanganyika inafaidi kuliko Zanzibar?
    Ipo dhana nyingine kuwa Zanzibar inanyonywa ndani ya Muungano na Tanganyika inafaidi ndani ya Muungano. Kinachostaajabisha, pia wapo wanaosema Tanganyika inanyonywa na Zanzibar inafaidi. Zote hizi ni hoja ambazo msingi wake ni husuda, na husuda haiondolewi na idadi ya serikali. Watu wenye husuda wataendelea kuwa na husuda hiyo ndani ya serikali moja au tatu.


    Wenye kuunga mkono dhana ya Zanzibar kunufaika kushinda Tanganyika wanatumia mifano ya haki ya kumiliki ardhi, makazi na mgawanyo wa madaraka wanaoupata wananchi wa Zanzibar. Ni kweli kuwa Wazanzibari wengi (inasadikiwa si chini ya laki nne) wanaishi Bara, wakimiliki ardhi na nyumba.


    Aidha, Wazanzibari wanashikilia nyadhifa kwenye wizara na sekta zisizo za Muungano kama afya na mawasiliano. Ni kweli pia Watanganyika nao wanashikilia nyadhifa nyingi kwenye wizara na sekta za Muungano na Watanganyika wanashikilia ajira nyingi kwenye sekta ya utalii Zanzibar. Isitoshe, wafanyabiashara wa Tanganyika wanauza bidhaa nyingi Zanzibar.Kilicho dhahiri ni kuwa hakuna upande wa Muungano ambao haufaidiki kabisa kutokana na uwepo wa Muungano. Sina shaka, manufaa hayo yaweza kupishana kutokana na maumbile yenyewe ya nchi hizi mbili. Mathalani, Watanganyika hawana tatizo kubwa la ardhi kiasi cha kuathirika kwa kukosa ardhi Zanzibar.


    Kupata ardhi ya makazi Zanzibar yaweza kuwa taabu kwa Mtanganyika lakini sio ardhi ya uwekezaji, maana hata wawekezaji kutoka nje hupata ardhi Zanzibar. Tukirejea kwenye takwimu za ujazo wa watu Zanzibar kwa kilometa ya mraba, ni dhahiri kuwa tayari Zanzibar kuna tatizo la ardhi, sio tu kwa Mbara, hata kwa Mzanzibari mwenyewe.
    Hivyo, dhana ya kuwa upande mmoja unanufaika na mwingine haunufaiki ni potofu. Pande zote zinanufaika, pengine, upo uwezekano wa kunufaika zaidi ikiwa tutarekebisha mifumo ndani ya muundo wa serikali mbili zilizopo.

    III. Nje ya Muungano Zanzibar itanufaika zaidi, Tanganyika itatua mzigo

    Ipo dhana kuwa nje ya Muungano, Zanzibar itanufaika zaidi na Tanganyika itatua mzigo. Wenye kujenga dhana hii, hujenga hoja kuwa Zanzibar itaweza kujenga ushirikiano wake yenyewe na dunia na nchi za kiarabu na kiislamu zenye uchumi imara. Wengine huzungumzia Zanzibar kuja kuwa bandari huru kama ilivyo Singapore. Tanganyika au Muungano huonekana kuwa ni kikwazo kwa Zanzibar kujiunga na Jumuiya ya Nchi za Kiislamu (OIC). Tunazidi kuaminishwa kuwa kwa kujiunga OIC, Zanzibar itajikwamua na umasikini.


    Waumini wa Tanganyika wanatuaminisha kwamba nje ya Muungano, Tanganyika itakuwa imetua mzigo. Hawa wanataka tuamini kuwa Zanzibar inaielemea Tanganyika na kwamba gharama za kuendesha Muungano zingeliweza kutumika kwenye miradi ya maendeleo. Wanatuaminisha kuwa Tanganyika imekuwa ikibeba gharama hizi peke yake na kwamba Tanganyika itaendelea kwa kasi sana, baada ya kuachana na Zanzibar.Dhana hii kuwa Zanzibar itanufaika nje ya Muungano ni dhana mufilisi na potofu. Hoja kwamba Zanzibar itaneemeka kwa kujiunga OIC ni ya kusadikika. Visiwa vya Comoro vina ukubwa wa kilometa za mraba 2170, vina idadi ya watu 984,500 na ni mwanachama wa OIC na Jumuiya ya Kiarabu (Arab League).


    Visiwa vya Comoro vingali masikini kuliko Zanzibar na ukuaji wake wa uchumi kwa mwaka 2012 ulikuwa asilimia 2.7. Tunachokipata hapa ni kuwa sio OIC wala Arab League yenyewe inayoweza kubadili uchumi na maisha ya Mzanzibari.
    Uchumi wa Zanzibar kama ilivyo Comoro kwa muda mrefu umefifishwa na migogoro ya kisiasa. Zanzibar ina tabaka kubwa la wanasiasa na utawala kuliko uwezo wa uchumi kuhimili, hivyo migogoro ya kisiasa haiepukiki. Nje ya Muungano, wanasiasa wengi wa Zanzibar watakosa ajira, hawa watajiunga na siasa za ndani za Zanzibar, hapatatosha. Migogoro ya kisiasa baina ya visiwa huko Comoro ina athari kubwa kiuchumi kuliko migogoro ya kisiasa baina ya Unguja na Pemba kutokana na siasa hizo kumezwa na siasa za Muungano.


    Isitoshe, nje ya Muungano, Tanganyika na Zanzibar zote kwa pamoja zitalazimika kubeba mzigo wa kugharimia ulinzi na usalama pamoja na uendeshaji wa ofisi za balozi nje ya nchi. Gharama hizi zikigawanywa kwa kila nchi kuendesha mambo haya yenyewe ni kubwa kwa kila nchi.
    Pengine tunapofushwa na gharama za kifedha pekee na kuacha kuangalia gharama za kiusalama. Usalama wa Zanzibar na Tanganyika unategemeana sana na Muungano ni chombo muhimu cha kuhakikisha usalama wa pande zote mbili.
    Tanganyika itagharimika sana kiusalama nje ya Muungano kuliko tunavyofikiria, hususan katika kipindi ambacho Tanganyika inatarajia kuvuna gesi katika pwani ya Bahari ya Hindi. Mahasimu wa Tanganyika watakuwa wamepata upenyo mzuri wa kutimiza azma yao ya kuidhuru Tanganyika au mahasimu wa Zanzibar kuidhuru Zanzibar. Hivyo, ustawi wa Zanzibar na Tanganyika unategemeana, wala sio kweli kuwa yuko mmoja anayembeba mwenzake au atakayekuwa salama zaidi nje ya Muungano.


    IV. Wazanzibar, Watanganyika wengi hawataki Muungano
    Wanasiasa wetu wa pande mbili wasioupenda Muungano kwa sababu wanazozijua wao, wanatuaminisha kwamba Muungano umechokwa na Watanzania wa pande zote mbili. Wanasiasa hawa hawa walifanikiwa kutushawishi kuwa Watanzania wengi wanataka Katiba mpya. Takwimu za waliojitokeza mbele ya Tume kutoa maoni juu ya Katiba mpya ni za kushitua. Katika nchi ya wapiga kura wanaokadiriwa kufikia milioni 20 kwa mujibu wa Tume ya Uchaguzi, waliojitokeza kutoa maoni yao hawakufika laki tano. Aidha, mwamko mdogo ulioonyeshwa katika ushiriki wa mabaraza ya Katiba unaacha maswali mengi.


    Wanasiasa na wanaharakati hutumia shinikizo kama mojawapo ya nyenzo kufikia malengo yao. Mojawapo ya nyenzo wanayoipenda sana ni kutumia umma kuhalalisha matakwa yao. Kwa sababu hiyo haishangazi kwa wanasiasa kupenda kutumia njia ya maandamano na lugha ya ‘wingi’ katika kujenga hoja zao. Kwa mbinu hii, lugha ya ‘wingi’ imetumika kutuaminisha kwamba Wazanzibari wengi hawautaki Muungano, hali kadhalika, Watanganyika wengi hawautaki Muungano.


    Lugha ya jumla imetumika pia kujenga dhana kuwa wanachama wa CUF wote hawaupendi Muungano, Wapemba wote ni CUF na Waunguja wote ni CCM na wanaupenda Muungano tena wa serikali mbili. Hali kadhalika, tunaaminishwa kuwa wanachama wa CHADEMA wote wanapenda serikali tatu na wanaCCM wanapenda serikali mbili.Katika kunogesha dhana yenyewe, inajengwa hoja kwamba, iwapo kura ya maoni ya kutaka au kutotaka Muungano itapigwa, basi haitapatikana theluthi mbili Zanzibar, kwa kuwa katika matokeo ya uchaguzi uliopita, hakuna chama kilichopata theluthi mbili ya kura.


    Wanaoshabikia dhana hii wanawachukulia wananchi kama misukule. Wanaamini wananchi watapiga kura kwa mlinganyo ule ule hata kama jambo ambalo wanalolipigia kura limebadilika. Kwa kutumia dhana hii, tunakatishwa tamaa ya kuutafuta ukweli kwa kuwapa fursa wananchi ya kuchagua iwapo wanautaka Muungano au hawautaki, wanataka serikali mbili au tatu. Hata Tume ya Katiba imetuingiza katika mkenge huu kwa kutuambia kuwa ‘wengi’ waliohojiwa wametaka serikali tatu. Hatujaambiwa waliotaka serikali mbili wangapi na waliotaka moja wangapi. Tunatakiwa tukubaliane tu kuwa wengi hawautaki Muungano pande zote mbili.
    Dhana hii haiakisi hali halisi. Wazanzibari na Watanganyika wameoleana, kuzaliana na wengine wanaendesha biashara kwa ubia. Ukisikiliza Sauti ya Radio Zanzibar katika taarifa za vifo utastaajabu kuwa karibu kila msiba una ndugu na jamaa Bara, tena sio Dar es Salaam pekee.

    Ukikaa katika Bandari ya Dar es Salaam au Zanzibar utashangazwa na idadi ya wasafiri kutoka pande zote mbili za Muungano. Wananchi wa kawaida wa pande zote mbili hawana tatizo na Muungano maana hauathiri maisha yao ya kila siku zaidi ya kuyarahisisha.


    Hawa, haswa wafanyabiashara, wanazo kero zinazohusiana na mifumo ya kodi zaidi kuliko muundo wa Muungano, au Muungano wenyewe. Hapana shaka, watakapoulizwa juu ya uwepo au kutokuwepo kwa Muungano, uamuzi wao utakuwa tofauti, kwa kuwa hatma ya Muungano ina athari kubwa sana kwao. Ni vyema tukaruhusu kura ya maoni juu ya uwepo au kutokuwepo kwa Muungano. Kura hii ya maoni, itatukwamua kutoka kwenye tope la wanasiasa, ambao ndio kero kuu ya Muungano.


    V. Muungano umepitwa na wakati

    Waswahili husema, ukitaka kumuua mbwa mpe jina baya. Ukimuita mbwa koko au kichaa unapata uhalali wa kumuua. Ukimpa jina zuri unamuhamishia sebuleni. Katika kutimiza azma yao, wale wasioupenda Muungano hutoa dhana ya Muungano kupitwa na wakati. Kwao suala la Muungano huchukuliwa kama tukio la kupita na sio suala la kudumu.

    Hivyo, tunatakiwa tuamini kuwa Muungano wetu umepitwa na wakati, na ulikuwa na mantiki tu wakati ule wa vita baridi na umajumui wa Afrika (Pan-Africanism). Zama hizo zimepita na hivyo Muungano nao umepitwa na wakati.


    Hoja hii nayo inajibika. Muungano wowote unaingiwa kwa lengo la kuwa Muungano wa kudumu. Chini ya sheria za kimataifa, uko msingi kuwa nchi huingia mkataba kwa dhamira njema ya kuutekeleza. Hivyo, Muungano wetu kama ilivyo miungano mingine ikiwemo ule wa Marekani na Ujerumani, inadhamiriwa kuwa ya kudumu.

    Tukirudi kwenye hoja yenyewe, Muungano wetu haujapitwa na wakati, labda baadhi ya viongozi wetu wamepitwa na wakati. Taifa letu linapita katika dunia ya utandawazi. Katika dunia ya utandawazi, nchi zinachukuliwa kuwa ni masoko. Muelekeo wa dunia ni kuunganisha nchi kuelekea kwenye utaifa mkubwa zaidi na si kinyume chake. Nchi ndogo zina nafasi finyu katika dunia ya utandawazi hususan pale nchi zenyewe ndogo zinapokuwa masikini.


    Nchi za Ulaya zinafanyia kazi wazo la kuungana kuwa nchi moja chini ya Umoja wa Ulaya. Nchi ya Ubeligiji yenye pato kubwa la uchumi kuliko jumla ya nchi zote kusini mwa Jangwa la Sahara inajiunga na nchi nyingine za Ulaya kujenga utaifa mkubwa kukabiliana na utandawazi. Aidha, tunaona jinsi ambavyo nchi zenye watu wengi kama India, China na Brazil zinavyotikisa katika utandawazi kutokana na kuwa na idadi kubwa ya watu. Ni kichekesho kuwa sisi nchi masikini tunafanya kinyume chake. Tunadanganyana kuwa tunayo fursa ya kuneemeka zaidi katika utandawazi tunapokuwa nje ya Muungano. Ukweli ni kuwa hatujiimarishi kwa kuwa nje ya Muungano bali tunajidhoofisha. Muungano unahitajika zaidi katika dunia ya utandawazi kuliko tunavyojifariji.


    VI. “Sisi” ni muhimu kuliko “Wao”

    Tunalo tatizo la kimtazamo miongoni mwa Watanganyika na Wazanzibari ambalo kwa maoni yangu msingi wake ni ubaguzi. Iko dhana ya ‘sisi’ na ‘wao’. Wananchi wa kila upande wamepandikizwa mitazamo dhidi ya wenzao wa upande mwingine. Baadhi ya Wabara huwaona Wazanzibari kama watu goigoi na huwaita ‘yakhe’ au ‘mdebwedo’.

    Hali kadhalika baadhi ya Wazanzibari huwaona Wabara kama watu wa shamba na wasiostaarabika, huwaita ‘machogo’. Mitazamo hii imeathiri kwa kiasi kikubwa uhusiano baina ya wananchi wetu, lakini baya zaidi, imetulewesha kwa kutupa majivuno kuwa ‘sisi’ ni bora kuliko ‘wao’.


    Athari kubwa itokanayo ni mitazamo hiyo ni kujenga kutokuaminiana. Wabara wanadhani Wazanzibari wote ni wazembe, hawana uwezo wa kiakili. Wazanzibari hali kadhalika wanawaona Wabara kama watu wasiostaarabika, wenye majivuno na kupenda kuburuza. Matokeo yake, mitazamo hii huambukiza vizazi na vizazi.

    Wananchi wa Zanzibari na Tanganyika waliopata bahati ya ama kuishi au kusoma na wenzao wa upande wa pili, watakubaliana nami kuwa mitazamo hii ni potofu. Binafsi, nimesoma na Wazanzibari na kufanya kazi na wale wenye uwezo mkubwa sana kushinda Wabara. Kama ilivyo kwa Wabara, tunao Wazanzibari wengi nje ya nchi kwenye mashirika ya kimataifa wanaotujengea heshima kubwa.


    Changamoto ya kimfumo iliyopo ni kwamba, kutokana na wingi wa Wabara, wengi wao hujikuta hawajawahi kufika wala kuishi Zanzibar, isitoshe, hawajawahi kusoma ama kuishi na Wazanzibari. Hivyo, wanasiasa hutumia mwanya huo kupandikiza mitazamo ya ‘sisi’ na ‘wao’ katika kutafuta kujijenga kisiasa.

    Maoni yangu ni kuwa, ‘sisi’ sio bora kuliko ‘wao’, wala ‘wao’ sio bora kushinda ‘sisi’. Wazanzibari, kama walivyo Watanganyika wamelifia taifa letu la Tanzania katika kulinda na kutetea heshima na uhuru wake. Watanganyika na Wazanzibar wamekufa katika vita vya Uganda wakipigania taifa letu.


    Majuzi, Watanganyika na Mzanzibari wamekufa huko Darfur wakiwa katika shughuli za kulinda amani. Maadui waliowaua wanajeshi wetu kule Darfur hawakutofautisha Mzanzibari wala Mbara, waliua wanajeshi wa Tanzania katika jeshi la kulinda amani la Umoja wa Mataifa. Haya yanayotuunganisha, ni muhimu zaidi, kuliko yale yanayotugawa.

    Mwalimu Nyerere katika hotuba yake ya ‘Nyufa’ aliyoitoa 1995 alionya juu ya dhana hii ya ‘sisi’ na ‘wao’. Katika hotuba ile, alikumbusha kuwa kinachotufanya tuwe ‘sisi’ ni kutokana na ‘wao’ kuwepo. Akaonya, ikiwa ‘wao’ hawapo, basi hata ‘sisi’ hatupo. Sote kwa pamoja ni bora zaidi kuliko ‘sisi’ au ‘wa

KWA HISANI YA

    Rai Mwema