MAKUNDI ya watu wenye ulemavu wa viungo mbalimbali wakiwemo wenye ulemavu wa miguu na macho mkoa wa Njombe wameiomba serikali kuwapatia nakala za katiba inayopendekezwa ili nao waweze kuzisoma na kuipigia kura rasimu hiyo ifikapo Aprili 30 mwaka huu ambapo hadi sasa awajafanikiwa kuiona.
Akizungumza na Elimtaa mkoani Njombe Mwenyekiti wa Chama Cha Walemavu Tanzania Mkoani humo CHAWATA Jakson Fihanga alisema kuwa makundi hayo ya watu wenye ulemavu wa viungo yamesahaulika kupatiwa rasimu hizo ili yaweze kutoa mchango wao katika katiba inayopendekezwa na kwamba hawafahamu ni wapi kwa kuipata
Alisema kuwa ukiwa umebaki mwezi mmoja lakini walemavu hao bado hawajafanikiwa kupata katika hizo inayo pendekezwa na kuisoma ili kuipigia kura.
Fihanga alisema kuwa swala la kuisoma katiba inayopendekezwa kwa walemavu wote wa mkoa wa Njombe ni mhimu na walipaswa kusoma na kuielewa ambapo hakuna kitabu hata kimoja cha alama za kusoma watu wenye ulemavu wa macho.
Alisema kuwa kutokuwapo kwa kitabu cha kuosoma watu wenyeulemavu wa macho ni jambo ambalo linaonesha dhahiri kuwa makundi hayo yatashindwa kuipigia kura Katiba hiyo pendekezwa.
Kwa upande wake katibu wa chama cha walemavu wasioona Daudi Mbanga alisema kuwa haki ya makundi ya watu wenye ulemavu ya kuipigia kura katiba inayopendekezwa haitatendeka endapo makundi hayo hayatahusishwa kwenye zoezi la kuipigia kura.
Mbanga alisema kuwa kutokana na makundi hayo kutopata nakala za katiba inayopendekezwa wanatarajia kwenda kwa mkurugenzi wa halmashauri ya mji wa Njombe ili kupatiwa ufafanuzi zaidi kwa nini makundi hayo yamesahaulika
Nao baadhi ya wananchi mjini Njombe walisema kuwa hata wao bado hawajafanikiwa kuisoma katiba inayopendekezwa kutokana na nakala kuwa chache jambo ambalo linawafanya watu wengi kushindwa kuisoma yakiwemo makundi ya walemavu.
Katiba pendekezwa inataraji kupigiwa kura ifikapo Aprili 30 licha ya kuwa inategemea kukamilika kwa zoezi la uandikishaji wa wananchi katika daftari la kudumu ambalo mpaka sasa halijakamilika katika mkoa mmoja wa Njombe kwenda kwa kusuasua.
Kauli za viongozi wa juu wamekuwa na msimamo wa kuwa kura hiyo ni razima Aprili 30 huku daftari hilo likiwa bado limesalia katika halmashauri za mkoa wa Njombe na kwenda kwa kusuasua.