Na Bashir Yakub
Wiki iliyopita niliandika kuhusu Asilimia kumi ambayo serikali za mitaa huwa wanaidai hasa maeneo ya mijini baada ya wahusika kuwa wameuziana nyumba au kiwanja. Nikasema wazi kabisa bila kungata meno kuwa hiyo pesa iitwayo asilimia kumi au pesa nyingine yoyote mtu atakayolipa serikali za mitaa eti kwakuwa amenunua au ameuza eneo lake ni rushwa. Na leo nakumbusha na kusisitiza tena kuwa Watanzana wajue ukitoa pesa ile umetoa rushwa na huyo kiongozi wa serikali za mitaa uliyempa amepokea rushwa kwakuwa malipo hayo hayatambuliwi na hayaainishwi na sheria yoyote. Lazima ifike hatua haya mambo yaeleweke. Pia nimetahadharisha mara nyingi kuhusu umakini unaponunua kiwanja/nyumba na kueleza baadhi ya mambo ambayo ukiyafanya utakuwa umefanya manunuzi salama na utakuwa umeepuka migogoro na hata mgogoro ukitokea wewe hautapoteza. Anayetaka kusoma haya yaliyopita aandike neno MAKALA SHERIA kwenye google ataona makala hizo. Leo tena naeleza uhalali kisheria wa serikali za mitaa kusimamia mikataba.
( a ) KISHERIA HAIRUHUSIWI SERIKALI ZA MITAA KUSIMAMIA MAUZO YA NYUMBA/KIWANJA.
Kwanza nataka nieleweke wazi kuwa nazungumzia sana ununuzi wa nyumba /viwanja kwa kuona huruma jinsi watu wanavyopoteza umiliki wa maeneo yao waliyonunua kwa kuamini wameyanunua kihalali kumbe kuna nukta walizokosea katika taratibu za kimanunuzi na sasa zinawagharimu. Ninayosema hapo yanatokea karibia kila siku mahakamani. Watu wanalia lakini mda huo huna wa kumlilia.Nianze hivi kisheria Wakili ndio mtu ambaye anaruhusiwa kusimamia mkataba . Wakili ana vyeo vitatu, kwanza ni wakili, pili mthibitishaji wa umma ( notary public) tatu ni afisa wa viapo. Uwakili nao ni cheo katika vyeo alivyonavyo wakili. Vyeo viwili yaani uwakili na uthibitishaji wa umma ndivyo humpa mamlaka ya kusimamia mikataba. Hapa naongelea nyumba/viwanja lakini kimsingi vyeo hivi si tu humpa mamlaka ya kusimamia mikataba ya viwanja/nyumba lakini pia mikataba yote. Hakuna katka nchi hii sheria yoyote ambayo imemruhusu kiongozi wa serikali za mitaa kusimamia mkataba, uwe wa nyumba, mkopo au wowote ule hata wa mauzo ya baiskeli. Kama hakuna sheria hiyo maana yake ni kuwa kusimamia mikataba si kazi yao. Kwa maana hii hii narudia kusema na kusistiza kuwa hairuhusiwi serikali za mitaa kusimamia mauzo ya nyumba/kiwanja.
( b ) MKATABA WANGU WA MANUNUZI YA NYUMBA/KIWANJA UMESIMAMIWA NA SERIKALI ZA MITAA JE UNA HADHI GANI?.
Kama ndani kwako una mkataba wa manunuzi ya nyumba/kiwanja ambao ulisimamiwa na serikali za mitaa basi ujue kuwa mkataba huo hadhi yake ni sawa na umesimamiwa na jirani yako , ndugu yako au mtu mwingine yeyote unayemuamini ambaye amekusaidia kukamilisha mkataba. Tuache kuishi kwa mazoea hii ndiyo hali halisi kisheria. Mkataba wa mauzo ya nyumba/viwanja au mkataba mwingine wowote uliofanyika serikali za mitaa ni sawa na mkataba uliofanyika nyumbani kwako. Hiyo ndio hadhi au nafasi ya mkataba wa aina hiyo kisheria. Kiongozi yeyote wa serikali za mitaa anaweza kuwa shahidi yako ukiamua kumuita lakini lazima ujue kuwa ushahidi wake katika mkataba wako kisheria ni sawa na ushahidi wa mtu mwingine yeyote. Hakuna eti kwakuwa huyu au hawa ni serikali za mitaa kwahiyo wakionekana katika mkataba wangu ndio utakuwa na uzito na wenye kuaminika zaidi, hapana. Hawa kama utaamua kuwashirikisha maana hata kuwashirikisha nayo ni hiari yako wanaweza kuwa mashahidi sawa na shahidi ndugu yako au jamaa yako mwingine yeyote . Anayeufanya mkataba kuwa na uzito mbele ya macho ya sheria ni wakili na huyu ndiye aliyepewa kazi hii. Kwa hiyo wanunuzi wa viwanja/nyumba jihadharini kwakuwa serikali za mitaa kisheria hilo si jukumu lao. Wanayo majukumu yao lakini hili si miongoni mwa hayo. Watu wasifanyiwe utapeli serikali haisimamii mikataba ya watu binafsi. Kama serikali kuu haiwezi kusimamia mkataba kati Bakhresa na Mohammed enterprise hata serikali za mitaa hawezi kusimamia mkataba kati yangu na wewe. Nawatahadharisha zaidi wanunuzi kwakuwa upande wa ununuzi ndio upande wa kupoteza linapotokea tatizo.
( c ) USHAURI KWA WANUNUZI WA NYUMBA/VIWANJA.
Kama unataka kununua nyumba/kiwanja na unataka mkataba wako wa manunuzi uwe na nguvu na hadhi ya usimamizi wa kisheria basi epuka kuwatumia serikali za mitaa kufanya jambo hili. Serikali za mitaa wanajua vyema kuwa kusimamia mikataba ya kuuza na kunuua si katika majukumu yao isipokuwa kwakuwa hapa ndipo penye hela kuliko hata hizo posho zao wanazopewa na serikali kuu basi hawako tayari kulisema hili kwa mtu yeyote. Hili utakuja kulijua vyema ukishapata mgogoro wakati wao hawapo tena wameshaondoka na chao. Mikataba ya serikali za mitaa haina hadhi na wanasheria wanaichallenge sana mahakamani wakati wa migogoro kiasi cha kuonekana kama vile pengine hukufanya mkataba kabisa. Migogoro ya nyumba na viwanja ni mingi mno lakini wewe unaweza kuiepuka migogoro hiyo ikiwa utazingatia ushauri wa kitaalam na utaepuka kukurupuka unapotaka kununua kiwanja/nyumba. Leo nilitaka nikuhadharishe na hilo ndugu mpendwa.
MWANDISHI WA MAKALA HAYA NI MWANASHERIA NA MSHAURI WA SHERIA KUPITIA GAZETI LA SERIKALI LA HABARI LEO KILA JUMANNE , GAZETI JAMHURI KILA JUMANNE NA GAZETI NIPASHE KILA JUMATANO. 0784482959, 0714047241
bashiryakub@ymail.com
0784482959, 0714047241
bashiryakub@ymail.com