Wabunge kuandamana na Kenyatta ICC

Rais Uhuru Kenyatta akiwasili katika mahakama ya kimataifa ya ICC
Idadi kubwa ya wabunge nchini Kenya wanajiandaa kuandamana na Rais Uhuru Kenyatta katika mahakama ya kimataifa ya ICC,Uholanzi ambako anatarajiwa kuhudhuria kikao maalum kuhusiana na kesi inayomkabili katika mahakama hiyo.
Kenyatta ametakiwa kufika mbele ya mahakama hiyo tarehe nane mwezi huu huku kiongozi wa mashitaka Fatou Bensouda akilalamika kuwa Kenya imekataa kushirikiana na mahakama hiyo kuhusiana na ushahidi dhidi ya Kenyatta.
Mapema wiki hii, mahakama hiyo ya ICC ilitupilia mbali ombi la Rais Kenyatta, la kutaka kikao hicho cha Octoba 8 kuhairishwa au aruhusiwe kutumia video. Majaji wa Mahakama hiyo walimuagiza Uhuru kufika binafsi mbele yao.
Wabunge hao walifika mmoja baada ya mwingine na kupanga foleni ndefu kuanzia asubuhi kuomba viza huku baadhi yao wakidai kuwa takriban wabunge 100 tayari wamewasilisha maombi ya visa kusafiri Uholanzi.
Wengi wa waliowasilisha maombi yao Ijumaa, walikuwa kutoka upande wa serikali. Lakini mwandishi wetu wa BBC Emanuel Igunza alizungumza na Mbunge wa Upinzani Jenerali Joseph Nkaiserry ambaye pia atasafiri pamoja na Rais.
''Suala hili sio la mrengo mmoja wa bunge au mwingine. Rais ni kiongozi wa Kenya nzima na ingepaswa sisi sote kama watoto wa chi hii kuwa pamoja na yeye’ alisema Nkaiserry ambaye ni mbunge wa upinzani.
Mbunge wa Lagdera, Kaskazini Mashariki mwa Kenya Mohammed Shidiye alisema kesi hiyo ya ICC, sio swala la Kibinafsi kwa rais bali ni la kitaifa
''Tunaona kwamba rais wetu anadhulumiwa, taifa letu linadhulumiwa na shida zimekuwa nyingi sana, kesi hii ni mambo ya kuwadanganya Wakenya,'' aliongeza Shidiye
Msemaji wa rais hata hivyo alikataa kuithibitishia BBC iwapo Uhuru Kenyatta atasafiri kuelekea Hague.
Kenyatta anatuhumiwa kuhusika na kupanga ghasia za kikabila zilizosababisha vifo na kuwalazmisha maelfu ya watu kutoroka makwao kwa hofu ya kushambuliwa.
Kenyatta amekanusha madai hayo dhidi yake.
Yote hayo yalitokea baada ya uchaguzi mkuu mwaka 2007 uliozua ubishi katika ya serikali na upinzani kuhusu mshindi halisi wa uchaguzi huo ulioshindaniwa na aliyekuwa Rais Mwai Kibaki na kiongozi wa upinzani Raila Odinga.