Facebook yakiri kosa la 'udukuzi'


Facebook imesema kuwa itabadilisha ambavyo inafanya utafiti wake , lakini nusura mtandao huo uombe radhi kwa njia moja uliotumia kufanya utafiti na kuzua kero miongoni mwa watumiaji wa mtandao huo.
Mnamo mwezi Juni mtandao huo ulikosolewa kwa kutumia taarifa za wateja wake laki saba bila ya ridhaa yao.
Mtandao huo umesema haukuwa umejiandaa kwa ambavyo ulikaripiwa.
" tumepokea malalamishi na ukusoaji wa wateja wetu bila kinyongo, na kuanzia sasa tuko tayari kubadilisha ambavyo tunafanya utafiti wetu, '' ilisema taarifa ya mtandao huo.
Katika blogu moja afisaa mkuu mtendaji wa teknolojia Mike Schroepfer, alisema kampuni hiyo ingezingatia njia mbadala za kufanya utafiti wake.
Aliongeza kusema kuwa waligundua kuwa walikosa kuwasilisha sababu za kufanya utafiti huo na sababu za utafiti wenyewe.
Katika utafiti huo, Facebook ilidhibiti akaunti za watumiaji wake kwa wiki moja mwaka 2012 bila ya kuwaarifu ili uweze kuchunguza hisia walizokuwa nazo kufuatia taarifa walizopata kila mara.
Utafiti huo ilikuwa sehemu ya utafiti wa Facebook kwa ushirikiano na vyuo viwili vikuu.
Mtandao huo ulisema ulikuwa unachunguza hisisa za watumiaji wa mtandao huo kuhusu taarifa walizopokea na ikiwa zilibadili tabia za watumiaji mtandao huo baadaye.
Hata hivyo, kampuni hiyo ilikosolewa sana kwa kutumia taarifa binafsi za watu ili kupima hisia za watu na kuwafanya kuwa wenye huzuni.
Kujibu tuhuma hizo, Facebook imesema inaanzisha masharti mapya kuhusu ambavyo inawafanyia utafiti watumiaji wake.
Lakini haikusema ikiwa itawajulisha watumiaji kuwa inawafanyia utafiti wala kuwaomba idhini ya kufanya hivyo kabla ya kuanza utafiti wenyewe.