Malindi yalalamikia kadi za manjano


Na Ali Cheupe
Timu kongwe ya soka visiwani Zaznibar, Malindi ambayo inashiriki ligi kuu ya Grand Malt imelalamikia kitendo cha wachezaji wake kuonyeshwa kadi za manjano bila ya utaratibu.
 
Akizungumza na mwandishi wa habari hii kwa njia ya simu, kocha msaidizi wa Malindi Mohammed Shuberi almaarufu Babu Shube alisema kitendo cha kuonyeshwa kadi tano za manjano kwenye mchezo mmoja ni njama maalum iliyoandaliwa kwa lengo la kuidhoofisha timu yao.
 
"Yaani ni jambo la aibu mwamuzi anamuonyesha kadi mlinda mlango wetu eti kwa kutoa mpira nje ili mchezaji mwenzake atibiwe" alifoka Shuberi.
 
Babu Shube aliosema kufuatia kitendo hicho, uongozi wa timu hiyo umepanga kupeleka malalamiko kwa katibu wa Chama cha soka Zanzibar kwa lengo la kuangaliwa kwa kina kadhia hiyo.
 
Kwa mujibu wa Kanuni ya Soka visiwani hapa kifungu cha 16 d kinasema kuwa "Timu ambayo wachezaji wake wataonyeshwa kadi tano za manjano katika mchezo mmoja itatozwa faini ya Shilingi elfu hamsini (50,000/).