Siku moja baada ya kuapishwa kwa rais mpya wa Afghanistan Ashraf Ghani, serikali yake imetia saini mkataba mpya wa usalama na shirika la kujihami la NATO.
Mkataba
huo utaidhinisha zaidi ya wanajeshi elfu kumi na mbili, wengi wakiwa
wamarekani, kusalia nchini Afghanistan hata baada ya kumalizika kwa
kandarasi yao mwaka huu.Mkataba huo ulitiwa sahihi katika hafula iliyotangazwa moja kwa moja katika televisheni na mshauri wa maswala ya usalama wa kitaifa wa Afghanistan Hanif Atmar na balozi wa Marekani nchini humo Jim Cunningham, huku Rais mpya wa Afghanistan Ashraf Ghani akishuhudia.
Uhusiano kati ya Marekani na Afghanistan ulizorota kutokana na Rais aliyeondoka, Hamid Karzai, kukataa kutia sahihi mkataba huo.
China ya masharti ya mkataba huo, ni chini ya wanajeshi 10,000 wa Marekani wanaotarajiwa kubaki nchini Afghanistan ili kutoa mafunzo na msaada kwa wanajeshi wa taifa hilo.
Rais aliyeondoka Hamid Karzai alikataa kwa muda mrefu kusaini mkataba wa kuwaongezea wanajeshi wa Marekani muda wa kukaa huko, na hivyo kusababisha mvutano kati yake na Marekani.
Bwana Karzai alikuwa anasisitiza kuwa la muhimu zaidi ni kuanzisha mpango wa amani na kusitisha mapigano na wanamgambo wa Taleban.
Vikosi vya NATO vimekuwa vikipunguzwa nchini Afghanistan na taratibu kurudisha udhibiti wa usalama wa nchi hiyo kwa vikosi vya Afghanistan.