ZAIDI ya Wasyria 245,000 wanaishi katika miji ambayo imezingirwa na wanakabiliwa na matatizo makubwa ikiwa ni pamoja na upungufu wa chakula.
Hayo yamesemwa na mratibu wa misaada ya dharura wa Umoja wa Mataifa Valerie Amos mjini Kuwait leo katika mkutano wa wafadhili wenye lengo la kukusanya kiasi ya dola bilioni 6.5 kwa ajili ya Wasyria ambao wameathirika na mzozo wa vita nchini mwao, ambao umesababisha kuuwawa kwa zaidi ya watu 130,000 tangu Machi mwaka 2011.
Amos amesema kuwa hatua ya kuzingira miji imekuwa mbinu ya kivita ambapo maelfu ya watu wanazingirwa katika jamii zao wakiwa hawana chakula na wanashindwa kupata mahitaji muhimu. Lengo la mkutano huo la kupata dola bilioni 6.5 ni kubwa kuwahi kuwekwa na Umoja wa mataifa na kwa ajili ya kuwasaidia Wasyria milioni 13 ambao wameathirika na vita vya miaka mitatu sasa nchini humo.