Jeshi la Uganda limesema kuwa majeshi yake yamejiunga na jeshi la serikali ya Sudan kusini katika vita dhidi ya uasi kwenye taifa hilo changa duniani.
Msemaji wa jeshi la Uganda luteni kanali Paddy Ankunda amesema leo kuwa majeshi ya uganda yanasaidiana na vikosi vya serikali ya Juba kuwaondoa waasi katika mji wa Bor, mji muhimu karibu na mji mkuu juba ambao umeshuhudia mapigano makali tangu kuanza kwa mzozo huo katikati ya mwezi uliopita nchini Sudan kusini.
Maafisa wa Uganda wamekuwa wakikana kuwa majeshi ya nchi hiyo yamejiunga na mapigano, wakisema majeshi ya Uganda wamewekwa Sudan kusini kwa ajili ya kufanikisha zoezi la kuwaondoa raia.
Rais Yoweri Museveni wa Uganda amesema jana kuwa wanajeshi wa Uganda wameuwawa katika mapigano nchini Sudan kusini.
Akizungumza katika mkutano mjini Angola jana, Museveni amesema majeshi ya nchi yake yamekuwa yakipigana kulisaidia jeshi la serikali nchini Sudan kusini.
Nao wabunge wa Marekani wameeleza kufadhaishwa kwao jana kuhusiana na wimbi la ghasia nchini Sudan kusini ,na kuwekea alama ya kuuliza hatua ya marekani kuendelea kutuma mamilioni ya dola kuisaidia nchi hiyo.
na DW.DESwahili