Kerry aanza ziara ya siku tano katika Mashariki ya Kati

Waziri wa Mambo ya Nchi za Kigeni wa Marekani John Kerry yuko katika Mashariki ya Kati kujaribu kuunga mkono mkakati wa makubaliano ya amani baina ya Israel na Palestina. 
Kerry amewasili leo mchana mjini Tel Aviv, Israel, na alitarajiwa kufanya mazungumzo na Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu na Rais wa Palestina Mahmoud Abbas.
Mazungumzo hayo yaliyodumu miezi mitano na ambayo yanastahili kudumu miezi tisa, yanakaribia kutokota, kwa sababu ya hasira ya Wapalestina dhidi ya ujenzi wa makaazi unaoendelea kufanywa na Israel na mgogoro kuhusiana bonde la Jordan ,mashariki ya Ukingo wa Magharibi. Msemaji wa Ubalozi wa Marekani mjini Tel Aviv Geoff Anisman amesema mkakati unaotayarishwa na Kerry utayaangazia masuala yote ya msingi katika mgogoro huo baina ya pande hizo mbili, ikiwa ni pamoja na mji wa Jerusalem, mipaka, wakimbizi, makaazi pamoja na mipango ya usalama.