Jeshi la Sudan laendelea na juhudi za kuukomboa mji wa Bor

Jeshi la Sudan Kusini la SPLA, leo limesonga mbele katika mji wa Bor, unaodhibitiwa na waasi, wakati pande hizo mbili zinazohasimiana zikikutana nchini Ethiopia kwa mazungumzo ya amani yenye lengo la kumaliza machafuko yaliyodumu wiki tatu na kutishia kuitumbukiza nchi hiyo katika vita vya wenyewe kwa wenyewe. Pande zote mbili zimekubaliana kimsingi kuweka chini silaha lakini hakuna upande uliosema wazi ni lini yatasimamishwa mapigano hayo yaliyosababisha vifo vya zaidi ya watu 1,000 na kuwaacha wengine karibu 200,000 bila makaazi. Rais wa Salva Kiir ametangaza hali ya hatari katika majimbo ya Unity na Jonglei ambayo mji mkuu Bor ulitekwa mapema wiki hii na waasi wanaomuunga mkono makamu wa rais aliyefutwa kazi Riek Machar. Nchi jirani zinazosimamia mazungumzo ya upatanishi baina ya pande zinazozozana zimeonya kuwa kuendelea kwa mapigano Sudan kusini, kunaweza kuvuruga mazungumzo hayo ya Addis Ababa.