HUU NDIO UKWELI WA MAMBO . CHADEMA KUINGIA UCHAGUZI MKUU 2015 IKIWA DHAIFU

MWENYEKITI WA CHADEMA

SAFARI ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kuelekea katika uchaguzi mkuu wa 2015 imeelezwa kuwa ni yenye kutia shaka na kimetabiriwa kufika mwaka huo kikiwa dhaifu.
Mwenendo wa matukio ambayo umma umeendelea kuyashuhudia ndani chama hicho wiki hii, msingi wake ukiwa ni kuvuliwa uongozi Zitto Kabwe na kuvuliwa uanachama kwa Dk. Kitila Mkumbo na Samson Mwigamba, ndiyo yaliyoibua hisia za namna hiyo miongoni mwa umma na jamii ya wasomi walioko ndani na nje ya chama hicho.
Tayari baadhi ya wasomi na wanasiasa wenye ushawishi hapa nchini, wakiwemo viongozi wa kada mbalimbali, wamekwisha kukaririwa kwa nyakati tofauti wakieleza kuona hatari ya kifo inayokikabili Chadema, kutokana na uamuzi wake huo wa kuwavua uanachama makada wake wawili na kutishia kuchukua uamuzi kama huo kwa Zitto.
Ndani ya Chadema na katika Kamati Kuu ya chama hicho, baadhi ya wajumbe wake nao wamekaririwa kutoa kauli zinazoonyesha kuona hatari ya kifo inayokikabili chama chao.

Mbunge wa Iringa Mjini, Mchugaji Peter Msigwa, amekaririwa ndani ya Kamati Kuu ya chama hicho hivi karibuni, akisema kuwa ni heri chama hicho kipoteze Uchaguzi Mkuu wa 2015, lakini Zitto aondolewe.
Mbali na Msingwa, miongoni mwa wasomi wanaoheshimika hapa nchini, na makada wa chama hicho, Mabere Marando na Profesa Mwesiga Baregu, nao wametoa kauli za kukionya chama hicho juu ya uamuzi wake huo na kueleza hatari wanayoiona mbele.
Marando amesikika ndani ya Kamati Kuu ya chama hicho akisema kuwa, anaona mwelekeo ule ule wa NCCR-Mageuzi kuipata Chadema.
Ni kutokana na hilo, matukio ya hivi karibuni kabisa ya kutekwa na kujeruhiwa kwa Mwenyekiti wa chama hicho Wilaya ya Temeke, Joseph Yona, lakini pia kuzuka vurugu ndani ya Kamati Kuu na lile la wafuasi wa chama hicho walio katika pande mbili zinazopingana, kupigana nje ya Mahakama Kuu ya Dar es Salaam, ambako Zitto alikuwa akitafuta haki yake ya uanachama, yanafananishwa na yale yaliyopata kutokea ndani ya chama cha NCCR-Mageuzi kati ya miaka ya 1990 na 2000.

Inaelezwa kuwa miongoni mwa mambo ambayo yalichangia chama cha NCCR-Mageuzi, ambacho kilikuwa chama kikuu cha upinzani nchini kupoteza nguvu zake wakati huo, ni migogoro ya kiuongozi ambayo ilisababisha watu kutwangana hadharani, kama ilivyo sasa kwa Chadema.

Tayari Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, Jaji Francis Mutungi, amekitaka Chadema kujiepusha na vurugu na uvunjifu wa amani wakati kinapotatua mgogoro wake na aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu wake, Zitto Kabwe.

Wakati hayo yakitokea, huko Kigoma baadhi ya wananchi nao wamekaririwa wakieleza kufedheheshwa na kauli iliyotolewa na baadhi ya viongozi wa Chadema ya kumuita Mbunge wao kuwa ni Mbunge wa Mahakama na wametamka bayana kwamba iwapo Zitto atatimuliwa, chama hicho kisahau kuungwa mkono mkoani humo.

Askofu Mstaafu wa Kanisa la Anglikana anayetoka Mkoa wa Kigoma, Dk. Gerald Mpango, ambaye amekuwa mpenzi mkubwa wa siasa za mageuzi na ameshiriki mikakati mingi ya kuijenga Chadema, amesikika akisema kuwa hatua ya kumtoa Zitto haitakiacha salama chama hicho, licha ya kuwahi kufanya hivyo kwa Dk. Amani Kabourou na David Kafulila.

Wasomi ambao wameelezea matukio yanayotokea ndani ya Chadema, wameonyesha shaka kama chama hicho kitaweza kufanya vizuri katika uchaguzi mkuu ujao na kuonya kuwa kisipotafuta suluhu mapema, kuna dalili za kuanguka.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Mzumbe, Prosper Ngowi, aliliambia Gazeti hili kwamba nyakati hizi si sahihi kwa chama hicho kuweka kipaumbele migogoro.

“Katika hili naweza kusema kuwa hiki si kipindi kizuri kwa Chadema kulumbana, kwasababu kama tunavyofahamu kuwa tunaelekea katika kipindi cha uchaguzi mkuu mwaka 2015, nilitarajia Chadema kama chama kikubwa cha upinzani kingetumia muda huu kujiimarisha zaidi kiweze kufanya vizuri katika uchaguzi wa 2015.

“Priority (kipaumbele) yao kwa sasa kilitakiwa kiwe kuangalia namna nzuri ya kuweka mikakati imara ya kuongeza madiwani, kuchukua viti vingi zaidi katika uchaguzi wa serikali za mitaa unaotarajiwa kufanyika mwaka huu, lakini pia kushinda majimbo mengi zaidi na ikiwezekana hata katika nafasi ya urais,” alisema Profesa Ngowi.

Alisema anashangazwa na kitendo cha sasa cha kuweka malumbano kama kipaumbele chao, hali ambayo inawadhoofisha katika kupanga mikakati imara ya ushindi.

“Wataalamu wa masuala vya vyama vingi wanasema kuwa kila lengo kubwa la chama cha upinzani, ni lazima katika kutafuta hiyo dola kuwe na mipango ya muda mrefu, sasa naona kama Chadema, moja ya chama kikubwa cha upinzani wameacha kufanya hilo kwa sasa na wameweka nguvu kubwa katika kutafuta migogoro, jambo ambalo linaweza kuwaangusha,” alisema Profesa Ngowi.

Alisema mgogoro uliopo kwa sasa hawezi kusema mshindi ni nani, bali busara inapaswa kutumika kumaliza tatizo lililopo kuweza kupata mwelekeo mzuri kuelekea mwaka 2015.

“Naweza kusema kuwa bado wana nafasi ya kusuluhisha hadi kufikia uchaguzi wa serikali za mitaa na kuelekea uchaguzi mkuu ujao,” alisema Profesa Ngowi.

Kwa upande wake, Mhadhiri wa Chuo Kikuu Huria (OUT), Profesa Peter Maina, alisema mambo yaliyojitokeza yataifikisha Chadema 2015 ikiwa dhaifu.

Alisema mgogoro uliojitokeza mpaka Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto kukimbilia Mahakamani, umetokana na uongozi wa chama hicho kushindwa kutumia busara kutatua mgogoro huo mapema.

“Niseme tu kwamba kuna watu ndio wameufikisha huu mgogoro hapo ulipo, ilikuwa rahisi kutumia busara kuumaliza pale wenzake na Zitto (Dk. Kitila Mkumbo na Samson Mwigamba) walipokiri kuandaa waraka na kusema ulikuwa siyo kwa nia mbaya.

“Lakini kuna watu wazito ndani ya Chadema kama kina Profesa Safari, Mabere Marando na wengine walipoona jambo hili inasemekana waliomba suluhu ya haraka, lakini inaonekana kuna watu upande wa chama hicho hicho hawataki suluhu na matokeo yake ndiyo haya ya kupelekana Mahakamani,” alisema Profesa Maina.

Alisema kitendo cha kulumbana nyakati hizi ni kusababisha chama hicho kuingia katika uchaguzi mkuu kikiwa dhaifu.

“Huu ni wakati wao wa kutafuta suluhu, naamini chama hakitakufa, lakini kitafika katika uchaguzi mkuu kikiwa dhaifu, hakitakuwa na nguvu kama ya awali, lazima viongozi wa Chadema wafahamu kuwa wakati mwingine haraka haina faida, uharaka uliotumika kushughulikia mgogoro haukuwa na faida.

“Kwa mfano, angalia Katibu Mkuu wa chama, Dk. Willibrod Slaa alivyofanya kipindi kile, badala ya kusuluhisha mgogoro, yeye anakwenda jimboni kwa Zitto kufanya mkutano, hapa inaonekana dhahiri hakuwa na nia ya kuleta suluhu, bali kuendeleza mgogoro, nafikiri busara hazikutumika toka awali na ndiyo maana leo hii mgogoro umekuwa mkubwa,” alisema Profesa Maina.

Katika hatua nyingine, Profesa Maina alisema kauli ya mwasisi wa chama hicho, Edwin Mtei, ya kusema Zitto hatakiwi ndani ya Chadema, inakiumiza zaidi chama, kwani haionyeshi demokrasi katika chama.

“Kauli ya Mtei inazidi kuonyesha nia ovu waliyonao baadhi ya watu ndani ya Chadema, kusema Zitto akatafute chama siyo maneno ya kuonyesha ukomavu kidemokrasia, niseme kwamba Mtei yeye anakiumiza zaidi chama, huu siyo wakati wa kulumbana ni wakati wa kutafuta suluhu kurudisha heshima ya chama.

Akizungumzia kitendo cha Zitto Kabwe kukimbilia Mahakamani alisema mbunge huyo amefanya hivyo kujikinga kutokana na hatua zilizopangwa kuchukuliwa dhidi yake.

“Kitendo cha Zitto kukimbilia mahakamani si kitendo cha ajabu bali amekwenda sehemu aliyoona haki itatendeka dhidi yake, unapoona mambo yanafanywa na mpinzani wako na unaona unaweza usitendewe haki una haki ya kwenda Makahamani kwahiyo wanaosema kwamba Zitto amekosea si kweli kwasababu yeye si mtu wa kwanza kwenda Mahakamani,” alisema Profesa Maina 

Na Nijimambo