KITENDAWILI CHA KUTANGAZWA BARAZA LA MAWAZIRI KUTEGULIWA LEO


Balozi Ombeni Sefue.
Katibu Mkuu Kiongozi na Mkuu wa Utumishi wa Umma, Balozi Ombeni Sefue ambaye pia ni Katibu wa Baraza la Mawaziri, leo atazungumza na waandishi wa habari Ikulu, Dar es Salaam. 
Taarifa fupi iliyotolewa jana na Ikulu, ikiwa haina ufafanuzi wowote, wala kutaja ajenda za mkutano huo, ilisema Balozi Sefue atazungumza kuanzia saa 5 asubuhi. 
Mkutano huo hata hivyo, kulingana na muktadha wa kisiasa uliopo nchini, ndio unaotazamiwa na wengi kutangaza uteuzi wa mawaziri wapya uliokuwa ukisubiriwa kufanywa na Rais Jakaya Kikwete. 
Uteuzi huo unatokana na nafasi wazi 5 zilizopo katika Baraza la Mawaziri baada ya mawaziri watatu nafasi zao kutenguliwa, mmoja kujiuzulu na mwingine kufariki dunia. 
Aliyefariki dunia hivi karibuni akiwa kwenye matibabu Afrika Kusini, ni aliyekuwa Waziri wa Fedha, William Mgimwa huku aliyekuwa Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Khamis Kagasheki akijiuzulu nafasi yake. 
Mawaziri waliotenguliwa nyadhifa zao ni aliyekuwa wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk Emmanuel Nchimbi, wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Shamsi Vuai Nahodha na wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi, Dk David Mathayo David. 
Mawaziri hao wanne walikumbwa na kadhia iliyotokana na Operesheni Tokomeza Ujangili , ambayo haikufanyika vema na watendaji wao wa chini na kusababisha kashfa ya mauaji ya raia, majeruhi, udhalilishaji kijinsia  na mauaji ya mifugo. 
Hayo yalijibainisha katika Mkutano wa Bunge ambapo baadhi ya wabunge walilalamikia utekelezaji wa operesheni hiyo hata kusababisha Kamati ya Maliasili, Ardhi na Mazingira, chini ya Mbunge wa Kahama, James Lembeli kupewa jukumu la kufanya uchunguzi. 
Baada ya uchunguzi ikathibitishwa kuwapo kwa vitendo hivyo vilivyokiuka haki za binadamu na hatimaye Waziri mmoja kujiuzulu na watatu kutenguliwa uteuzi wao, huku mmoja akifariki dunia kwa ugonjwa na kusababisha nafasi hizo kuwa wazi. 
Watu mbalimbali wakiwamo wanasiasa, wanahabari na wachambuzi wa masuala ya kisiasa, walianza kubuni, kuzusha na wengine kuvumisha kufanyika kwa mabadiliko makubwa katika Baraza la Mawaziri huku wengine wakifikia hatua ya kubashiri majina. 
Hatua hiyo ilifanya ofisi ya Balozi Sefue kutoa tamko la kukanusha kuwapo uteuzi huo na kutaka wananchi kuvuta subira, kumwachia Rais afanye kazi yake kuhusu nafasi hizo. 
Kutokana na uvumi na uzushi huo, ulifika wakati zikaibuka tuhuma za baadhi ya ‘wanaowania’ uwaziri ambao hausomewi wala kugombewa, kujikuta katika mitego ya kurubuniwa na waliojifanya wana usalama wa Taifa na kuwakamua fedha ili “wawapigie debe wateuliwe.” 
Kwa kuwa nafasi za wazi zilizopo ni tano tu haitarajiwi Rais kuvunja Baraza lake na kuja na jipya, ila kinachotazamiwa ni kuziba mapengo yaliyopo na pengine kubadilisha nafasi. 
Lakini haitashangaza kuona baadhi ya waliotenguliwa nafasi zao wakirejeshwa kwenye uwaziri ingawa si katika nafasi zilezile, kwa sababu kutenguliwa kwa nafasi zao hakukumaanisha kwamba walishiriki moja kwa moja kukiuka haki za binadamu katika operesheni hiyo. 
Hata hivyo, hiyo haimzuii Rais kuingiza sura mpya katika Baraza lake pale atakapoona inafaa na baada ya kushauriana na wasaidizi wake wa karibu, ilimradi nia ni kuhakikisha maendeleo ya Mtanzania yanapatikana. 
Alipoulizwa kama upo uwezekano wa mkutano huo kutangaza mawaziri wapya, Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu, Salva Rweyemamu alikataa kujua undani wa mkutano huo, mbali ya kusema yeye alitakiwa kualika waandishi na si zaidi ya hapo. 
“Mimi niliombwa kufanya kazi ya kualika tu na Katibu Mkuu Kiongozi mwenyewe alisema atazungumza na waandishi na kama kuna maswali ataulizwa hapo hapo,” alisema Rweyemamu.
Na Matutukio na Vijana