Katibu wa CCM Mkoa wa Mjini Mwangi
Rajabu Kundya akimnadi mgombea wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Mahmoud
Thabit Kombo katika kampeni za uchaguzi mdogo wa Jimbo la Kiembesamaki
zilizofanyika Mbweni Wilaya ya Magharibi Unguja. (Picha na Makame
Mshenga wa Maelezo Zanzibar).
Mgombea Uwakilishi wa Jimbo la Kiembe
Samaki kwa tiketi ya chama cha Mapinduzi (CCM) Mahmoud Thabit Kombo
akiwahutubia wananchi waliofika katika kampeni zake Mbweni Wilaya ya Magharibi Unguja.(Picha na Makame Mshenga wa Maelezo Zanzibar).
Chama cha Mapinduzi ni chama chenye kuleta maendeleo ambacho kinapinga ubaguzi na kuwatetea wananchi haki zao za msingi
Hayo yameelezwa jana
huko Mbweni na Katibu wa CCM Mkoa wa Mjini Mwangi Rajab Kundya katika
kampeni za uchaguzi mdogo wa Jimbo la Kiembesamaki.
Amesema kuwa kuna
baadhi ya vyama vya upinzani vinachochea kuleta ubaguzi nchini kwa
kisingizio cha kutaka Zanzibar iwe na mamlaka yake kamili kinyume na
matakwa yao.
Aidha amesema kuwa
Zanzibar imeshapata mamlaka yake tangu baada ya Mapinduzi na kuundwa kwa
chama cha Afro Shirazi Party ASP ambapo tayari ina viongozi kamili na
sifa zake zote za kupata maamlaka hayo.
“Mamlaka kamili tayari yamepatikana tangu ilipoundwa ASP hivyo wanataka mamlaka gani tena”, aliuliza Kundya.
Amefahamisha kuwa CCM sio chama chenye kuleta ubaguzi kwa wananchi kwani kiko makini katika kuwaletea maendeleo ya nchi.
Amesema CCM ina viongozi makini ambao ni wataalam wa uongozi hawayumbishwi na watu wasiopenda maendeleo ya nchi.
“Kiongozi wa watu
lazima ajitie katika makundi ya watu ili aweze kujua shida zao kwa
lengo la kutatua matatizo ya watu wao lakini wapinzani hawana utaala
huo”, alifahamisha bwana Kundya.
Aidha Katibu huyo
amewataka wananchi wa Jimbo la Kiembesamaki kumchagua kiongozi wa CCM
kwani ndiye atakaeweza kusimamia Muungano, kupigania haki ya wanzibari
na maendeleo kwa jumla.
Nae mgombea uwakilishi
wa chama hicho Mahmoud Thabit Kombo ameahidi kuimarisha matawi ya CCM
kwa kinamama na jumuiya za wazazi pamoja na kuwaimarisha na
kuwashajihisha vijana katika mambo ya ajira.
Na Miza Kona – Maelezo