HATIMAYE mahakama ya hakimu Mkazi Mbeya, imewaachia huru raia
watatu wa Afrika Kusini (wawekezaji shamba la Kapunga), wilayani Mbarali, waliokuwa
wakikabiliwa na kesi ya kumwaga wiwatilifu vyenye sumu kwenye mashamba ya
wakulima yanayozunguka shamba hilo na kuangamiza
mazao yote yaliyomea.
Inadaiwa kuwa raia hao, Waldeman Veemark,Sergei Beacker na Andreas Daffee walimwaga
viwatilifu vyenye sumu katika mashamba ya wakulima yenye ukubwa wa hekari
557.5, Januari 24 mwaka 2012 baada ya kuibuka ugomvi baina yao.
Akisoma uamuzi wake jana, katika kesi hiyo ya jinai namba
43/2012, Hakimu Mkazi wa mahakama hiyo, Michael Mteite, alisema imewaachia huru
washitakiwa hao baada ya upande wa walalamikaji
kushindwa kuthibitishia kutendeka kwa kosa hilo.
“Baada ya kusikiliza na kuchambua ushahidi na vielelezo vilivyotolewa upande wa walalamikaji
chini ya jamhuri,mahakama hii imefikia uamuzi wa kuwaona washitakiwa wote
watatu hawana kesi ya kujibu, hivyo
inawaachia huru” alisema Mteite.
Aliongeza kuwa ushahidi wote uliotolewa Mahakamani hapo ni
dhaifu na kushindwa kuishawishi mahakama iwaone washitakiwa wana kesi ya
kujibu.
Alisema licha ya jamhuri kuwasilisha mashahidi 154, mashahidi 54 hawakuweza kufika mahakamani
hapo, huku tisa wakitoa ushahidi wa uwongo jambo lililoleta mashaka juu ya kesi
hiyo.
Pia jamhuri ilishindwa kuwasilisha ushahidi wa kisayansi ili
kuthibitisha aina ya sumu iliyotumika kuangamiza mimea yao ya mpunga
iliyoangamizwa kama ilivyoelezwa kwenye kesi hiyo.
Aliongeza kuwa, kitendo cha kushindwa kuwasilishwa kwa
ushahidi wa kisayansi licha ya sampuri zake kuchukuliwa na kupelekwa katika
maabala mkoani Arusha ni wazi kimesababisha kuona washitakiwa hawana kesi ya
kujibu.
Awali wakijitetea mbele ya mahakama, mshitakiwa namba moja, alisema
siku ambayo wakulima walisema kuwa waliiona ngege ikimwaka sumu hiyo ilikuwa ni
sikukuu ya kitaifa hivyo wao walikua mapumziko.
Alisema kutokana na hali hiyo yeye alishinda ofisini akijaza
taarifa mbalimbali hivyo si kweli kuwa alifanya tukio hilo, huku washitakiwa namba
mbili na tatu walidai kuwa kwa kuwa siku
hiyo ilikuwa ya mapumziko waliitumia kwenda kufanya manunuzi mjini Mbeya.
Hata hivyo, baada ya kumalizika kesi hiyo na kuacha maswali
mengi , wakulima hao walisema hawajakatishwa tamaa na wanatarajia kukata rufaa.