MAUAJI YA KUTISHA TUNDUMA



NI WATOTO WA DIWANI

MMOJA ACHINJWA KICHWA



WATOTO wawili wa familia ya diwani wa kata ya Nkangamo wilayani Momba mkoani Mbeya Weston Simwelu,wameuawa kikatili, huku mmoja akichinjwa na mwingine kwa kunyongwa shingo. .

Tukio hilo lilitokea Juzi nyumbani kwa diwani huyo, majira ya saa 8:00 na saa 9:00 mchana katika mtaa wa  Tazara uliopo mjini Tunduma wilayani Mbomba Mkoani Mbeya.

Akizungumzia tukio hilo diwani huyo aliwataja watoto hao kuwa ni Kalebu Simwelu (6) ambaye ni wakiume na alikutwa amechinjwa kwa kutumia kisu kikali kilichoachwa kikininginia shingoni kwa mtoto huyo.

Aidhaa alimtaja mtoto mwingine ambaye alikuwa mfanyakazi katika familia hiyo kuwa ni Sister Nyirenga (14) ambaye alikutwa amenyongwa kwa kutumia waya, mkanda na minati na hatimaye miili ya marehemu hao ilifichwa nyuma ya kochi ndani ya nyumba hiyo.

Akizungumza kwa majonzi diwani huyo alisema siku hiyo alikuwa yuko shambani na mke wake alikuwa kazini katika ofisi za halmashauri ya mji mdogo wa Tunduma,ambaye ndiye alikuwa wa kwanza kugundua mauaji ya mtoto wa kwanza baada ya kufika nyumbani...

Alisema baadaye mkewe huyoTumaini alimpigia simu na kufahamisha tukio hilo huku akijua kuwa mtoto wa kazi alikuwa akihisiwa kuwa amekimbia baada ya kufanya mauaji ya mtoto wao.

Simwelu aliongeza kuwa alipofika nyumbani hapo aligundua kuwa huyo mtumishi wa ndani naye ameuawa kwa kunyongwa na mwili wake kufichwa jirani na mwili wa mtoto wao nyuma ya kochi la kukalia

Kwa upande wao viongozi wa mji wa Tunduma Franck Mwakajoka na kiongozi wa mtaa huo Stansraus Malekela alisema kitendo hicho kuwa kimefanywa na watu wenye roho ya kinyama ya kuwauawa watoto wasiokuwa na hatia.

Walisema tukio hilo ni la kwanza kutokea katika mji huo hivyo waliitaka serikali iwasake wote waliofanya mauaji hayo kwa kuwa mji huo hali yake ya usalama imekuwa siyo nzuri.

Kaimu kamanda wa polisi mkoani Mbeya, Barakael Masaki amethibitisha ku tokea kwa mauaji hayo ambayo alisema kuwa  yametokea katika mazingira ya kutatanisha na hakuna mtu aliye amatwa kuhusiana na tukio hilo.

Alisema jeshi la polisi mkoani humo linaendelea kufanya uchunguzi zaidi kuhusiana na tukio hilo.

Na Bosco Nyambege Momba