Meya wa jiji la Mbeya Athanas Kapunga alitoa onyo hilo kwenye kikao cha balaza la madiwani wa halmashauri hiyo na kusisitiza kuwa timu ya Mbeya City ni ya wakazi wa jiji la Mbeya na si ya mwana siasa yeyote wala chama chochote cha siasa. Kwa kauli hiyo ni watu wengi huenda wakatafsiri kuwa meya huyo alikuwa akiwanyooshea kidole mbunge wa viti maalumu mkoa wa Mbeya Dk.Mary Mwanjelwa na pia mbunge wa Mbeya mjini Joseph Mbilinyi(Sugu) ambao wamekuwa wakishiriki mara kadhaa katika matukio mbalimbali ya timu ikiwemo kutoa fedha kuwawezesha mashabiki kuambatana na timu inapokwenda kucheza ugenini. Katika kikao hicho Kapunga alisema kuendeleza mbwembwe za kisiasa kunakofanywa na wanasiasa kunaweza kuisababishia timu kupoteza mwelekeo kwa wadau kugawanyika kwenye makundi yenye milengo tofauti ya kisiasa. “Yawezekana kuna watu hawajui historia ya Mbeya City.Hii si timu ya mwanasiasa yeyote wala chama chochote cha siasa.Sisi tuliomo humu yaani madiwani na wakazi wa jiji la Mbeya ndiyo wenye timu.Timu hii haiwahusu wabunge.Kama wataingia huko waje kama madiwani lakini si kutumia nguvu ya ubunge wao huku”
“Kwa wabunge wenyewe tumeanza kuwaona baada ya timu kufanya vizuri.Huko nyuma hatukumuona hata mmoja.Tumehangaika wenyewe mpaka imefikia hapa leo hii anakuja mtu anasema timu yangu.
Hilo hatulitaki.kama kuna mtu ameona kwenye timu ndiyo pa kujiongezea umaarufu wa kisiasa sisi hatutaki.”
Alisisitiza. Kwa upande wake Dk.Mwanjelwa aliyekuwepo kwenye kikao hicho alikiri kuwa kuingia kwa wanasiasa kwenye timu kunalenga kumnufaisha mtu binafsi kisiasa na kunaweza kuisababishia timu hiyo kuingia kwenye migogoro ya kisiasa.
NA LYAMBA LYA MFIPA