Waangalizi walaani unyanyasaji dhidi ya Wasomali baada ya Westgate



  Kufuatia ripoti ya mfululizo wa kukamatwa kusiko halali huko Eastleigh, viongozi wa dini na wachambuzi wa masuala ya usalama wanatoa wito kwa vikosi vya usalama vya Kenya kuacha kutumia shambulio la Westgate kama ruhusa ya kunyanyasa na kutisha watu wasio na hatia wa jumuiya za ndani za Wasomali na Waislamu.


  • Vikosi vya usalama vya Kenya vikiwa vimesimama nje ya kituo ya biashara cha Westgate huko Nairobi tarehe 26 Septemba, 2013. [Carl de Souza/AFP] Vikosi vya usalama vya Kenya vikiwa vimesimama nje ya kituo ya biashara cha Westgate huko Nairobi tarehe 26 Septemba, 2013. [Carl de Souza/AFP]
  • Polisi wa Kenya wakiondoa vizuizi vilivyokuwa vimewekwa barabarani wakati wa utezwaji dhidi ya Wasomali huko Eastleigh baada ya shambulio la kigaidi tarehe 18 Novemba, 2012. [Carl de Souza/AFP] Polisi wa Kenya wakiondoa vizuizi vilivyokuwa vimewekwa barabarani wakati wa utezwaji dhidi ya Wasomali huko Eastleigh baada ya shambulio la kigaidi tarehe 18 Novemba, 2012. [Carl de Souza/AFP]
Badala yake, kuimarisha ushirikiano na jumuiya hizo, kuongeza nia njema na kufanya kazi nao katika kukusanya taarifa za kipelelezi ni jambo muhimu, wasema, kuimarisha nchi na kuzuia mipango ya kigaidi ya baadaye.
Bado wakati na baada ya uzingiraji wa siku nne wa mwezi uliopita uliofanywa na al-Shabaab katika kituo cha maduka ya biashara cha Westgate huko Nairobi, vikosi vya usalama viliripotiwa kulenga Waislamu na watu wenye asili ya Somalia kwa kuwaweka kifungoni na kuwahoji.
"Nimekuwa mwathirika siyo mara moja bali mara mbili," alisema Ali Omar mwenye umri wa miaka 24, wa kabila la Kisomali ambaye anaishi katika eneo linalojulikana kama Majengo jirani na Eastleigh ya Nirobi. "Kila wakati kunapokuwa na shambulio, wote tunachukuliwa kama washukiwa, nyumba zetu zinapekuliwa, tunaingizwa kwenye magari ya polisi na kupelekwa vituo kadhaa vya polisi ambapo tunapewa adhabu na kupigwa kwa uhalifu tusioujua."
Omar alisema polisi waliwazingira yeye na rafiki zake wawili wakiwa wanatembea kurudi nyumbani wakitiokea kwenye swala ya jioni tarehe 22 Septemba, siku moja baada ya uzingiraji kuanza. Watu hao watatu walifungwa kwa siku tatu pasipo kufunguliwa mashtaka, aliiambia Sabahi.
"Matukio kama hayo yanatufanya tutishike ambapo hata kama tungekuwa na taarifa zozote ambazo zingekuwa muhimu katika kuwakamata wahalifu, tungeamua kunyamaza kwa sababu wakati wote sisi ni washukiwa namba moja," Omar alisema.
Siku hiyo hiyo wakati polisi walipowachukua Omar, Fatuma Musa, mama wa watoto watano, alisema maofisa walipekua nyumbani kwake huko Eastleigh na walimchukua kijana wake wa kiume mwenye umri wa miaka 16 kumweka chini ya uangalizi.
"Timu ya maofisa wa polisi ilikuja usiku. Walisema walikuwa wanaangalia mabomu na walipoipekua nyumba yote [hawakuweza] kupata kitu chochote," Musa aliiambia Sabahi, akiongeza kwamba polisi walimshikilia kijana wake kwa kumuhoji kwa siku moja kabla hawajamwachia.

Kutafuta ukweli, kujenga uaminifu

Wakitiwa wasiwasi na hadithi hizo, viongozi wa Waislamu wanayaomba mashirika ya ulinzi kutotumia mashambulizi ya magaidi kama kisingizio cha kuwanyanyasa watu wasio na hatia.
Sheikh Khalfan Khamis, mwenyekiti wa Baraza la Wanazuoni Waislamu nchini Kenya, aliyalaani mashambulizi ya al-Shabaab katika Westgate, lakini alisema ni makosa kwa polisi kuwaadhibu Waislamu wote kwa makosa yaliyofanywa na magaidi.
"Serikali inapaswa kutafuta ukweli na kuwataja wahalifu hao wanaohusika na uhalifu huo wa kutisha na kuheshimu haki za wasio na hatia wakati ikifanya hivyo," aliiambia Sabahi.
Kuwasumbua watu wasio na hatia kuhusiana na makosa ambapo wao nao ni waathirika kunaleta ugumu wa mapambano dhidi ya ugaidi, alisema Mustafa Ali, katibu mkuu wa Baraza la Viongozi wa Dini Afrika, shirika ambalo linalenga kutatua migogoro na kudumisha amani katika Afrika kupitia ushirikiano baina ya dini mbalimbali.
"Wakati wowote tunapokuwa na mlipuko katika mji, polisi wanaoshughulikia wanafanya uvamizi kwa wakaazi wa Eastleigh," Ali aliiambia Sabahi. "Kitu kinachotokea ni kufanya ugumu wa kukusanya wapelelezi, kwa vile wenyeji hao wangependa kujitolea taarifa nzuri za kutumia kuwakamata watuhumiwa hawafanyi hivyo."
Alisema ugaidi ni tatizo la kiusalama na kijamii ambalo linahitaji jitihada kubwa kutoka kwa jamii na mashirika ya ulinzi kulikabili.
"Lakini hata wakati viongozi wa dini na jamii wanaelezwa kama magaidi, inajenga kutoaminiana na chuki kati ya mashirika ya ulinzi na wananchi. Watu wanachagua kukaa na kuangalia upande mwingine wakati hali inakuwa mbaya," alisema, akiwashauri viongozi kufuata mikakati ya polisi jamii ya kujenga uaminifu na uzalendo.
Mwenyekiti wa Chama cha Biashara cha Wilaya ya Eastleigh Hassan Gulleid alisema hivyo kufuatia mashambulizi ya Westgate, wakaazi walikuwa katika mshtuko na kuogopa kushirikiana na mashirika ya ulinzi.
"Ugaidi ni tatizo ambalo linaleta uharibifu usio na maana kwetu sote na hauwezi kufumbiwa macho," aliiambia Sabahi, akitaja umuhimu wa kujenga uaminifu na heshima baina ya jamii na vikosi vya usalama. "Kitu pekee kinachohitajika ni ushirikiano kutoka kwa kila mmoja wetu katika jamii hii ili kuweza kuutokomeza. Lakini ushirikiano huu hauwezi kulazimishwa wala kushurutishwa."
Kwa hivyo, Chama cha Biashara cha Wilaya ya Eastleigh kimeandaa programu za kuwafikia ambako mashirika ya ulinzi yamealikwa kushirikiana na vijana wa Eastleigh kupitia shughuli za michezo, kuanzisha njia nzuri za mawasiliano ambazo zitakuza uelewa na ushirikiano.
Kama chama cha biashara, alisema, wanatoa pia chanzo cha utafutaji riziki kwa vijana ambao vinginevyo watakuwa wakishawishiwa na waajiri wa al-Shabaab kwa kuwaahidi fedha.
Simiyu Werunga, kapteni wa jeshi la Kenya ambaye pia ni mkurugenzi wa Kituo cha Afrika cha Mafunzo ya Kimkakati, alisema mashirika ya ulinzi yanapaswa kujihusisha na idadi ya watu na kujenga ushirikiano imara pamoja na jamii ya Kiislamu.
Kutumia nguvu nyingi katika kuchagua jamii kunatelekeza watu na baadaye kuwatenga, kunawafanya kuwa katika mazingira hatari zaidi katika msimamo mkali, aliiambia Sabahi.
Ni mkakati usiofaa, alisema, sio tu kwa sababu unazuia jitihada za kukutana kiintelijensia, lakini pia inaweza kuwasaidia al-Shabaab katika kuajiri. "Hii sio njia ya kukabiliana na ugaidi." alisema.

Serikali yajibu

Kwa upande wake, serikali ya Kenya ilikataa kukosolewa kwamba maofisa polisi wamekuwa wakiwanyanyasa Wasomali na Waislamu katika ghasia za shambulizi la Westgate.
"Sijui lolote kuhusu unyanyasaji wa watu wasiokuwa na hatia huko Eastleigh," Katibu wa Mambo ya Ndani na Uratibu wa Serikali ya Taifa Joseph Ole Lenku aliiambia Sabahi. "Kwa jinsi ninavyoelewa, timu yetu ya maofisa wa polisi wanafanya [uchunguzi] kitaalamu."
Yeyote aliyenyanyaswa na wanajeshi wa usalama anapaswa kuripoti kwa mamlaka huru ya kusimamia polisi, alisema.
"Kile ambacho tumekuwa tukifanya ni kuwakamata wale tuliowashuku kuwa na uhusiano na mashambulizi, kuwahoji na kuwaachia ambao hawana hatia, na huu ndio utaratibu kwa dunia nzima," alisema Lenku.
Mamlaka pia zinawafikia wananchi ili kuwasaidia katika uchunguzi, alisema, akiagiza wananchi wote kuwa sehemu ya suluhisho la ugaidi kwa kujitokeza na taarifa zozote zinazohusiana na shughuli zenye utata.