Takribani watu sita wameuawa na wengine zaidi ya 22 kujeruhiwa wakati mlipuaji wa kujitoa mhanga alipoligonga gari la jeshi la Afghanistan lililokuwa limeweka ulinzi katika eneo ambapo viongozi wa kisiasa na makabila wanatarajiwa kukutana wiki ijayo kujadili kuhusu mpango wa usalama wa nchi hiyo pamoja na Marekani.

Karibu viongozi wa makabila na kiraia 2,500 wanatarajiwa kushiriki katika kikao hicho kinachofahamika kama "loya jirga" Alhamisi wiki ijayo, ili kuamua kama watakubali rasimu ya muafaka huo wa makubaliano kuhusu usalama baina ya Afghanistan na Marekani. Rasimu ya mpango huo iliandaliwa mjini Kabul mwezi uliopita, wakati wa ziara ya Waziri wa Mambo ya Nchi za Kigeni wa Marekani John Kerry.
Taliban, ambao waliangushwa na operesheni ya kijeshi iliyoongozwa na Marekani mwaka wa 2001, wamepinga mkutano huo wakiwaonya wafuasi wao kuwa wataadhibiwa kama "wasaliti" ikiwa watauidhinisha mpango huo wa usalama.