Rais wa Sri Lanka hataki uchunguzi
Rais wa Sri Lanka, Mahinda
Rajapakse, ameutoa maanani kwa ukali wito wa waziri mkuu wa Uingereza,
David Cameron, kwamba wajumbe wa kimataifa wachunguze madai ya uhalifu
uliofanywa mwisho wa vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini humo,
vilivyomalizika mwaka 2009.
Akizungumza katika mkutano wa viongozi wa nchi
za Jumuia ya Madola mjini Colombo, Rais Rajapakse alisema wafanye wao,
wakifanya wenzao huwa mwao ("wanaoishi kwenye nyumba za vigae hawafai
kuwarushia mawe wengine.")
Katoa kauli hiyo baada ya Bwana Cameron, ambaye
anahudhuria mkutano huo, kusema kuwa Uingereza itahimiza kufanywe
uchunguzi wa kimataifa iwapo Sri Lanka yenyewe haikuanzisha uchunguzi
usiopendelea upande wowote.
Alitaja safari ya Bwana Cameron siku ya Alkhamisi katika eneo la Jaffna liloharibika wakati wa vita.
Bwana Rajapakse alisema aliruhusu wageni wake kuzuru eneo la kaskazini kwa sababu Sri Lanka ni nchi huru.