8047942_orig
 Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe akifafanua jambo wakati vyama vya upinzani vya Chadema, NCCR-Mageuzi na CUF vilipokutuna  jijini Dar es Salaam na kutoa tamko la ushirikiano juu ya mustakabali wa mchakato wa katiba mpya, baada ya kupitishwa kinyemela kwa muswada wa marekebisho ya sheria ya mabadiliko ya katiba. Kushoto ni Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia na Mwenyekiti wa CUF, Prof. Ibrahim Lipumba.  (Picha na Francis Dande)

-CHADEMA, NCCR na CUF zaungana kutembea nchi nzima kuelezea mapungufu ya rasimu ya Sheria ya Marekebisho ya Katiba Mpya.
Vyama vya siasa vya CHADEMA, NCCR-Mageuzi na CUF vimetamka kuungana na kushirikiana juu ya mustakabali wa mchakato wa katiba mpya, baada ya kupitishwa kwa muswada wa marekebisho ya sheria ya Mabadiliko ya Katiba.
Viongozi  wakuu wa vyama hivyo Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia na Mwenyekiti wa CUF, Prof. Ibrahim Lipumba, wakizungumza na wanahabari jijini Dar es Salaam ili kufikisha ujumbe wao kwa umma walisema kuwa muungano huo umemuomba Rais Jakaya Kikwete asiusaini muswada wa mabadiliko ya Katiba wa mwaka 2013, uliopitishwa na bunge hivi karibuni kwa kuwa una mapungufu.
930448009
Mwenyekiti wa CUF, Prof. Ibrahim Lipumba akisisitiza jambo.
Viongozi hao wamesema vyama hivyo vinaanza kuunganisha umma kufanya maamuzi ya kuunusuru mchakato huo wa kwa kufanya mikutano nchi mzima kuanzia Jumamosi ijayo, ambapo mkutano wa kwanza utafanyika katika Viwanja vya Jangwani, mjini Dar es Salaam.
Akitoa tamko la vyama hivyo mbele ya waandishi wa habari, jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahimu Lipumba, alisema wanamuomba Rais aurejeshe muswada huo bungeni ili ufanyiwe marekebisho ambayo ndiyo yatakuwa yenye kujenga na kuaminiana.
Alisema vyama vyao vimeamua kuunda ushirikiano na kuweka pembeni tofauti zao ili kuunganisha nguvu za pamoja kwa maslahi ya taifa.
Profesa Lipumba alisema vyama hivyo vinalaani ukiukwaji wa kanuni za Bunge ambao ulifanywa wa kuingiza vifungu vipya kinyemela. Alisema vyama hivyo vinahisi nguvu za wananchi na wadau mbalimbali zinapaswa kuunganishwa kuunusuru mchakato huo.
Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe akiunga mkono tamko hilo alisema wataidai Katiba Mpya kwa gharama yoyote na wataitafuta kwa njia yoyote na wako tayari kufanya kazi na mtu yoyote.
IMG_9942
Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia aliunga mkono tamko hilo kwa kusema anatambua kwamba vyama vyao vina tofauti kubwa za kitikadi lakini vinaungana kwa ajili ya Katiba.
Baada ya kuzungumza na Waandishi wa habari, viongozi wa vyama hivyo walikutana na Wahariri katika chumba hicho kwa mazungumzo ya takribani dakika 20 na kisha kupata chakula cha mchana kwa pamoja.