RUNGWEl: CHANGAMOTO KUONDOLEWA CHUO CHA MSASANI

HALIMASHAURI ya  Wilaya ya  Rungwe  Mkoani Mbeya itaondoa changamoto zilizopo kwenye chuo cha ualimu  Msasani  ikiwamo ya kujenga shule ya sekondari katika chuo hicho ili kuwarahisishia wanachuo katika chuo hicho kufanya mazoezi ya kufundisha kirahisi kuliko ilivyo hivi sasa.
Mkuu wa wilaya ya Rungwe, Crispine Meela.
Kauli hiyo ilitolewa  hivi karibuni na mkuu wa Wilaya ya Rungwe Chrispin Meela wakati wa mahafari ya 36 ya kuwaaga wanachuo waliohitimu kozi ya Diploma ya Ualimu iliyofanyika katika ukumbi wa chuo hicho uliopo kata ya Msasani Wilayani humo,
Meela  ambaye alikuwa mgeni rasmi katika mahafari hayo alisema kuwa kawaida ya vyuo vya ualimu ni kuwa na shule za sekondari ili kurahisisha masomo ya vitendo yatakayo warahisishia wanafunzi  kufanya vizuri katika masomo yao na kupelekea kuwa na waalimu wenye sifa katika Idara ya elimu,
‘’Changamoto zote zilizotolewa hapa nitazifanyia kazi na kipaumbele ni kujenga shule ya sekondari ya chuo kwa lengo la kupunguza usumbufu wanaoupata wanafunzi ambao wanasafiri umbali mrefu kwenda kufanya mazoezi  ya  kufundisha katika shule za mbali’’ alisema  Meela,
Alizitaja  changamoto zilizopo chuoni  hapo kuwa ni  uchakavu wa majengo,mfumo mbovu wa maji  katika vyoo,ubovu wa barabara yenye kilometa 3 kutoka chuoni hadi Tukuyu mjini,ukosefu wa shule ya sekondari  pamoja na upungufu wa nyumba za waalimu ambapo alisimia 80 ya waalimu wanaishi kwenye nyumba zilizopo mbali na shule hiyo,na Serikali imekubali  kuondoa changamoto hizo,
Mkuu wa chuo hicho Mathius Mvula mbali na kuipongeza Serikali kukubali kuondoa changamoto hizo pia alitaja idadi ya wahitimu wa mwaka huu kuwa ni 491 kati ya hao wanaume ni 313 na wanawake ni 178,na kuongeza kuwa serikali inatakiwa kukitazama kwa jicho la tatu chuo hicho ambacho kinatoa  waalimu wengi wa masomo ya Sayansi  na sanaa  kwa  zaidi ya miaka sita sasa,
Aliongeza kuwa chuo hicho kinapokea wanafunzi wengi lakini majengo yaliyopo chuoni hapo ni chakavu yanatakiwa  kufanyiwa ukarabati  na kuwa  iwapo  serikali itaondoa changamoto zilizopo sifa za  chuo hicho zitaongezeka na kwamba kwa sasa hali ya chuo hicho haiendani na taaluma nzuri wanayoitoa kwa kuwa majengo yaliyopo ni  chakavu na yanashusha hadhi ya cho hicho,
Mkuu huyo  wa chuo alimaliza kwa kuwaasa wahitimu  kuwa makini na maisha ya uraiani kuacha kujiingiza katika vitendo viovu,na kuwa  iwapo watapangiwa kufanya kazi ya kufundisha katika shule zilizopo vijijini wasikatae kwani imekuwa ni kawaida ya waalimu kuzikataa shule za vijijini na kuzikimbilia shule zalizopo mijini na kuziacha shule za vijijini zikiwa na upungufu mkubwa wa waalimu.