SAKATA la walimu wa shule
ya Sekondari ya Forest Jijini Mbeya kugeuza chumba cha darasa kuwa uwanja wa
mateso kwa wanafunzi limeingia sura mpya baada ya walimu waliokamatwa na
Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) kuachiwa kwa dhamana na
kurejea kazini.
Kufuatia hatua hiyo jana
Wanafunzi wa kitato cha nne katika shule hiyo waligoma kuingia madarasani
wakishinikiza waalimu hao washughulikiwe.
Wanafunzi hao waligoma
baada ya kuwaona waalimu hao wakirejea shuleni hapo kufundisha huku wao
(wanafunzi) wakiona kuwa hakuna dalili yoyote ya walimu hao kuwajibishwa.
Baada ya kuanza kwa mgomo
huo, Afisa Elimu wa Mkoa wa Mbeya, Juma Kaponda alifika shuleni hapo na
kuwataka wanafunzi hao waingie madarasani wakati Serikali ikiendelea kushughulikia
madai yao.
Kapomda alisema kuwa
Takukuru bado wanaendelea kufanyia kazi tuhuma za rushwa zinazowakabilio walimu
hao na baada ya kukamilisha uchunguzi wao watawafikisha mahakamani.
Alisema kuwa kwa vile
walimu hao bado hawajafikishwa mahakamani, kisheria hawawezi kusimamishwa kazi,
hivyo akawataka wanafunzi kuendelea kuwa wavumilivu hadi pale uchunguzi wa
Takukuru utakapokuwa umekamilika.
“Waalimu hawa
hawatasimamishwa kazi mpaka watakapo fikishwa mahakamani, hivi sasa Takukuru
inaendelea kulifanyia kazi suala hili na ninyi tunaomba muendelee kuwa
wavumilivu,” alisema Kaponda.
Kaponda alisema kwa sasa
waalimu hao wataendelea kufundisha mpaka watakapobainika kuwa wana kesi ya
kujibu na hapo ndipo hatua za kinidhamu dhidi yao pia zitakapochukuliwa.
Alisema kuwa mbali na
kuwapinga walimu wao, wanafunzi hao pia wamekuwa na madai mengine mawili,
ambayo ni kupewa vitambulisho na wasiwasi wa kuendelea kupewa kibano na walimu
wao.
Alisema walimu
waliolalamikiwa watakuwa watuhumiwa mpaka pale mahakama itakakapowatia hatiani
baada ya kesi yao
kufunguliwa na Takukuru.
“Kuna taratibu za
kiserikali kwamba Takukuru itakapo wapeleka mahakamani ndipo na sisi
tutawasimamisha kazi, lakini kabla kesi
haijaenda mahakamani hatuwezi kuwasimamisha kazi,” alisema Kaponda.
Kaponda waliwataka
wanafuzni hao kuwa wavumilivu, wenye subila na waendelee na masomo bila
wasiwasi kwani tatizo lao liko kwenye hatua nzuri ya kufanyiwa kazi.
Waalimu hao walikamatwa na
Takukuru Februari 4 mwaka huu wakituhumiwa kuwatoza fedha wanafunzi wanaochelewa
ili wasiwaadhibu kwa viboko.
Inadaiwa kuwa walimu hao
walikuwa wametenga chumba kimojawapo cha darasa kuwa sehemu maalumu kwa ajili
ya kuwasulubu wanafunzi, chumba ambacho kilipewa jina la Guantanamo.
Kwa mujibu wa wanafunzi
hao, ni kwamba mwanafunzi anayeingizwa ndani ya chumba hicho husulubiwa kwa
bakora na kisha kuinamishwa kichwa chini miguu juu kama
sehemu ya adhabu.