MAPAMBANO dhidi ya rushwa yameendelea
kushika kasi Mkoani Mbeya, baada ya Taasisi ya Kuzuia na kupambana na rushwa
nchini (Takukuru) Mkoani hapa, kuwanasa walimu wawili wa shule ya Sekondari
wakiomba rushwa kwa wanafunzi wachelewaji.
Walimu hao
ni wa shule ya sekondari ya kata ya Forest ya Jijini hapa,ambao inadaiwa kuwa
walikamatwa na taasisi hiyo kwa tuhuma za kushawishi na kupokea rushwa ya kati
ya shilingi 500 na 1,000 kwa wanafunzi wanaochelewa kufika shuleni asubuhi.
Akizungumza
na waandishi wa habari ofisini kwake jana, Kamanda wa TAKUKURU mkoani hapa,
Daniel Mtuka, alisema Tukio hilo lilitokea jana Jijini hapa, majira ya saa 8:30
kufuatia baadhi ya wanafunzi wa shule hiyo kutoa taarifa na taasisi hiyo
kuweka mtego.
Mtuka
aliwataja walimu hao kuwa ni Solomoni Mwasote na Faustin Robert ambao walitiwa
mbaroni shuleni hapo na kukutwa na kiasi cha shilingi 64,000 walizokuwa
wamezikusanya kutoka kwa wanafunzi hao huku pembeni kukiwa na fimbo nyingi
zilizokuwa zikitumika kuwachapia wanawafunzi hao.
Mtuka
alisema kutokana na wingi wa wanafunzi shuleni hapo idadi inayofikia wanafunzi
900 kwa siku lazima wanafunzi wasiopungua 300 ni lazima wachelewa kufika
shuleni hivyo kwa siku walikuwa wanakusanya fedha kiasi kisichopungua 150,000.
“Hapa
ukiangalia walimu walikuwa wamejiwekea mtandao mkubwa wa mradi hebu fikiria
shule ina wanafunzi 900 na wote wanakaa nyumabi kwao hivyo lazima kuna
wanafunzi wanaochelewa kufika shuleni hapo ambao hawapungua 300 na kwa siku
walimu wanajikusanyia fedha kiasi kisichopungua shilingi 150,000 kwa siku.
Alisema kuwa
wanaendelea ana mahojiano na walimu hao na baada ya hapo watuhumiwa hao
watafikishwa mahakamani.
Kamanda
Mtuka alisema kuwa walimu hao wamekuwa na mradi huo wa kuwalipisha wanafunzi
ambapo alidai kuwa walimu hao walikuwa wamejiwekea mtindo huo kwa kipindi
kirefu ambapo wanafunzi wanaochelewa walikuwa wanaambiwa watoe fedha kuanzia
shilingi 500 hadi shilingi 1000 ndipo asichapwe na kama mwananfunzi hana hiyo
fedha ndipo anapochezea kichapo cha viboko visivyokuwa na idadi kutoka kwa
walimu hao.
“Walikuwa
wamejiwekea mradi wa kuwatoza wanafunzi wanaochelewa kufika shule kiasi cha
fedha kuanzia shilingi 500 hadi 100 ili asichapwe viboko lakini mwanafunzi kama
hana hiyo fedha basi analazimika kuchezea viboko visivyokuwa na idadi,”alisema
na kuongeza:
“ Kwanza
walimu hao walikuwa wanachukuwa majina ya wanafunzi waliochelwa kutoka kwa
walimu walioko zamu na kuanza kuwaita kwenye chumba walichokuwa wanakiita
‘Gwantanamu’ na kuanza kutozwa fedha hizo”alisema Kamanda Mtuka.
Hata hivyo
timu ya waandishi wa habari waliolazimika kufika shuleni hapo kwa lengo la
kuongea na wanafunzi pamoja na uongozi wa shule, baadhi ya wanafunzi hawakusita
kuongelea kitendo hicho walichokuwa wakifanyiwa na walimu hao.
Mwanafunzi
Shafii Israel wa kidato cha kwanza, alisema kuwa mwanafunzi ambaye hana fedha
za kuwapatia alikuwa anaambiwa ainame kichwa chini miguu juu kisha
mwalimu huyo anamchapa kwa kufuata uti wa mgongo.
Alisema
baada ya kuona kitendo hicho kinaendelea huku uongozi wa shule ukiwa
umekaa kimya tukaamua kuwambia viongozi wa serikali ya wanafunzi ndipo
walipokwenda takukuru.
Mkuu wa
shule hiyo, Cecilia Kakela, alipotakiwa kuzungumzia sakata hilo kwa waandishi wa
habari alikata kabisa kuzungumzia huku akijibu majibu mawili tu kwamba hajawahi
kuviona vitendo na hajui lolote.