KANISA la Waadventista Wasabatho (SDA)
linalomiliki Shule ya Sekondari Ndembela wilayani Rungwe limeamuliwa kuondoa
shule hiyo kwenye majengo na ardhi inayomilikiwa na wananchi wa Kijiji cha
Ndembela, kata ya Makandana wilayani Rungwe.
Uamuzi huo ulitolewa juzi na Mkuu wa Wilaya ya Rungwe, Chrispine
Meela wakati akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Ndembela kwa ajili ya
kusuluhisha mgogoro huo uliodumu kwa muda mrefu.
Kwa zaidi ya miaka 16 sasa
kumekuwepo na mgogoro baina ya kanisa hilo na wananchi wa kijiji cha Ndembela
kuhusiana na umiliki wa shule hiyo ambayo awali ilikuwa ya umma lakini mwaka
1994 ikakabidhiwa kwa kanisa hilo ili waiendeshe.
Akifafanua kuhusu sakata hilo, Meela alisema kuwa baada ya
Serikali kuikabidhi shule hiyo kwa uongozi wa Kanisa la SDA, pia kanisa
liliruhusiwa kuifanyia usajili, hivyo shule hiyo ni mali halali ya kanisa hilo.
Hata hivyo Meela, alisema kuwa ardhi na majengo ya shule
hiyo bado ni mali halali ya Serikali ambayo kwa niaba yake inapaswa kusimamiwa
na wananchi wa kijiji cha Ndembela.
“Shule ya Sekondari Ndembela kama
taasisi ni mali halali ya Kanisa, lakini properties (mali) kama vile majengo na
ardhi ni mali ya umma na hivyo tunalitaka kanisa liondoe shule yake kwenye
majengo na ardhi ya umma,” alisema Meela.
Alisema awali wananchi walifanya
makosa kudai shule hiyo na ndiyo sababu kesi ilipopelekwa mahakamani, mahakama
iliamua kuwa shule ni mali ya kanisa, lakini kama suala lingekuwa ni mali,
hakuna shaka kuwa wananchi wangepewa ushindi.
Awali akisoma risala ya wananchi
hao, mmoja wa wakazi wa kijiji hicho, Dornad Mwakasaka, alisema kuwa wananchi
hawana haja na shule hiyo, isipokuwa wanataka warejeshewe ardhi na majengo yao
ili wayatumie kwa maslahi yao na vizazi vijavyo.
Alisema kuwa wananchi hao wametumia njia za amani kudai haki hiyo
kwa miaka zaidi ya 16 na sasa wameanza kuishiwa na uvumilivu na kuwa wako
tayari hata kumwaga damu ili kuhakikisha wanarejesha ardhi na majengo hayo
mikononi mwao.
“Tumefuatilia haki yetu hii kwa muda mrefu lakini tunapuuzwa na
Serikali, huku Kanisa hili likizidi kukalia ardhi na majengo yetu kwa nguvu,
sasa tumeishiwa na uvumilivu na kama hatupati suluhu sasa tutatumia nguvu ya
umma kurejesha mali yetu,” alisema Mwasaka.
Baada ya Hotuba ya Mkuu wa wilaya, wananchi hao walionyesha
kufurahishwa na uamuzi huo, hivyo kuweka kando hasira na mipango yao ya kuvamia
shule hiyo kwa lengo la kuwatimua kwa nguvu viongozi wa kanisa hilo.