WANANCHI wilayani Rungwe
wamefurahishwa na uamuzi wa Serikali wa kufuta utaratibu wa kuwatumia mawakala
kusambaza pembejeo za ruzuku kwa wakulima wilayani humo, kwa madai kuwa utaratibu
huo haukuwa na tija kwa wananchi masikini.
Kauli ya wananchi hao imefuatia
tangazo la Mkuu wa Wilaya hiyo Chrispine Meela kuwaeleza wananchi kuwa Serikali
imeufuta mfumo huo na badala yake ruzuku itatolewa kupitia kwenye vikundi vya
wananchi ambavyo vitapewa mikopo isiyokuwa na riba za kibiashara.
Mkuu wa wilaya ya Rungwe Chrispine Meela |
Meela alitoa tangazo hilo juzi
kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika katika Kijiji cha Ndembela kilichopo kata
ya Makandana wilayani humo alikokuwa akizungumza na wananchi.
Meela aliwataka wananchi hao kuanza
kuunda vikundi vidogo vidogo ili fedha za ruzuku zitakapotolewa na Serikali
waweze kukopeshwa na kuzitumia kununulia pembejeo za kilimo kwa ajili ya msimu
ujao wa kilimo.
Wakizungumza na Nipashe baada ya
tangazo hilo la Mkuu wa Wilaya, wananchi hao walisema kuwa mfumo wa kusambaza
mbegu na mbolea za ruzuku kwa kuwatumia mawakala uliwakandamiza watu masikini
na wale wasiokuwa na uwezo wa kujieleza kwenye vikao vya kamati za mbolea za
vijiji.
Dornald Mwasaka (61) alisema kuwa
amefurahishwa na uamuzi wa Serikali wa kufuta utaratibu wa kusambaza mbolea kwa
kuwatumia mawakala kwa sababu mawakala walikuwa wakichakachua vocha za ruzuku
hali ambayo ilisababisha mbolea isiwafikie walengwa.
“Baadhi ya mawakala badala ya
kuleta mbolea walikuwa wakija kununua vocha kwa bei nafuu kutoka kwa wakulima na
kuzipeleka benki, hali hiyo ilisababisha mbolea isifike vijijini, kwa kweli
nimefurahishwa kuona utaratibu huo umefutwa,” alisema Mwasaka.
Mwananchi mwingine, Yusta Bulambo
alisema kuwa utaratibu mpya uliotangazwa na Mkuu wa Wilaya anaona ni mzuri ingawa
wananchi bado hawajahamasishwa vya kutosha kujiunga kwenye vikundi.
“Nikiangalia hapa kijijini kwetu
hakuna vikundi hivyo vinavyosemwa, ingawa utaratibu mpya unaonekana ni mzuri,
lakini wasiwasi wangu ni kwamba bado sisi wananchi hatujaanzisha vikundi
vinavyotakiwa na hivyo tunaweza kunyimwa fedha za mikopo kwa kutotimiza
mashariti ya kujiunga kwenye vikundi,” alisema Bulambo.
Kwa upande wake Diwani wa Kata ya
Makandana, Boniphas Mwasikili alisema kuwa utaratibu mpya utawasaidia wananchi
wake kupata mbolea kwa kuwa utaratibu wa zamani ulikuwa na dalili za ubaguzi.
“Katika utaratibu wa Vocha, kamati
ya Mbolea ndiyo ilikuwa inachagua watu wa kupewa ruzuku, sasa hapo inawezekana
kamati ikachagua kwa ubaguzi, lakini sasa kwa sababu mbolea itatolewa kwa
mkopo, kila mwananchi mwenye uwezo ataipata,” alisema Diwani Mwasikili.