MWANZA: BIL. 3.2 ZAKUSANYA NA PPF
MFUKO wa Pensheni wa Kuhudumia Mashirika ya Umma (PPF) Kanda ya Ziwa, umefanikiwa kukusanya zaidi ya sh bilioni 3.2, ikiwa ni fedha za michango ya wanachama, zinazotolewa na waajiri mbalimbali katika mikoa ya ukanda huo.
Fedha hizo zimekusanywa kwa kipindi cha kuanzia Januari hadi Mei mwaka huu, na kwamba PPF imeboresha zaidi huduma kwa wateja wake kwa lengo la kuwavutia wananchi wengi zaidi kujiunga.
Meneja wa PPF Kanda ya Ziwa, Meshack Bandawe, ameyasema hayo wakati akiwasilisha taarifa ya maendeleo ya mfuko huo katika kikao cha Kamati ya Ushauri ya Maendeleo Mkoa wa Mwanza (RCC).
Amesema makusanyo ya michango hiyo yanatokana na waajiri kuzingatia elimu inayotolewa mara kwa mara na viongozi wa mfuko huo, kuhusu umuhimu wa kulipa michango ya wanachama kwa wakati.
