DAR ES SALAAM: CHADEMA WAAHILISHA ZIARA KIFO CHA BOB NYANGA



CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kimelazimika kukatiza ziara yake ya kujiimarisha katika mikoa ya kusini kutokana na kifo cha mwasisi wake, Bob Nyanga Makani, kilichotokea usiku wa kuamkia jana.

Tayari viongozi wakuu wote wa chama hicho wamerejea jijini Dar es Salaam, kushughulikia taratibu za mazishi ya mwanasiasa huyo, aliyewahi kushika nyadhifa kadhaa katika Serikali ya Awamu ya Kwanza.

Akielezea msiba huo, Mkurugenzi wa Habari na Mawasiliano wa CHADEMA, John Mnyika, amesema kuwa wameupokea kwa majonzi makubwa kutokana na mzee huyo kuwa nguzo muhimu kwenye chama.

Makani ambaye alikuwa katibu mkuu wa kwanza na mwenyekiti wa pili wa chama hicho, amefariki muda mfupi baada ya kufikishwa katika Hospitali ya Aga Khan jijini Dar es Salaam saa 4.15 usiku, akisumbuliwa na maradhi ya kibofu cha mkojo na mapafu.