Kenya leo imeanza maombolezi ya kitaifa ya siku 3 kufuatia kifo cha Waziri wa usalama wa ndani Profesa George Saitoti na Naibu wake Orwa Ojode, waliofariki katika ajali ya Helikopta ilioanguka katika msitu wa Ngong jana .
Ajali hiyo ilitokea dakika chache baada ya kuondoka uwanja wa ndege wa Wilson katika ndege mpya ya polisi, wakielekea kwenye mkutano wa kuchangisha fedha katika jimbo la uchaguzi la Ndiwa aliokuwa akiliwakilisha marehemu Ojode kama mbunge.
Marubani wawili na walinzi wawili pia waliuwawa katika ajali hiyo, ambayo chanzo chake hakijajulikana. Polisi wanaendelea na uchunguzi wao.
