WAZIRI WA MAWASILIANI NA UCHUKUZI KUTOKA ZANZIBAR


KAMATI Teule ya Baraza la Wawakilishi iliyochunguza ubadhirifu serikalini, imetaka kuwajibishwa kwa aliyekuwa Waziri wa Mawasiliano na Uchukuzi, Machano Othman Said, baada ya kujihusisha na udalali wa kuuza kiwanja cha wizara kwa mfanyabiashara maarufu nchini, Said Bakhressa, kinyume cha sheria.

Machano ni Mwakilishi wa Jimbo la Chumbuni na ni Waziri wa Nchi asiye na Wizara Maalumu katika Serikali ya Umoja wa Kitaifa inayoongozwa na Dk. Ali Mohamed Shein.


Aidha, ripoti ya Kamati hiyo imewasilishwa katika Baraza la Wawakilishi, inataka kuchukuliwa hatua za kinidhamu kwa Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Dk. Lila, kwa kushindwa kusimamia mali za wizara kwa mujibu wa sheria wakati yeye ndiye msimamizi mkuu.


Akiwasilisha ripoti ya Kamati hiyo imepewa kazi ya kufanya uchunguzi kuhusu tuhuma za ubadhirifu serikalini kwa awamu, Mwenyekiti wake Omar Ali Shehe amesema walibaini kwamba Wizara ya Mawasiliano na Uchukuzi imefanya ubadhirifu mkubwa na kuitia hasara Serikali.


Katika uchunguzi huo, walibaini kwamba Machano amejishughulisha moja kwa moja na kugeuka dalali kwa kuuza kiwanja cha Wizara kwa Bakhressa kwa Sh milioni 200. Akifafanua, Mwenyekiti wa Kamati amesema uchunguzi ulibaini kwamba Waziri Machano ndiye aliyempigia simu Bakhressa na kumwambia kuna kiwanja kinauzwa.


Kwa mujibu wa Kamati hiyo, kiwanja hicho kiliuzwa na Waziri Machano, kwa bei ya ‘kutupa’ na kulikosesha Taifa fedha nyingi; hivyo kuitaka wizara kuhakikisha kinarudi mikononi mwa Serikali haraka.