BARAZA la Usalama
la Umoja wa Mataifa limeitaka Sudan
kusimamisha mara moja mashambulizi yake ya anga dhidi ya Sudan Kusini, katika
mgogoro unaoendelea baina ya nchi hizo kuhusu eneo la mpakani lenye utajiri wa
mafuta.
Maafisa wa ngazi
za juu wa Umoja wa Mataifa wamethibitisha kwamba mashambulizi hayo yameuwa
takribani raia 16 na kujeruhi wengine 34 katika jimbo la Sudan Kusini la Unity.
Baraza la Usalama
limetoa wito wa kusimamishwa mapigano hayo, na kuonya kuwa linaweza kuchukua
hatua zaidi mnamo siku zijazo, kuzuia kupanuka kwa mgogoro baina ya nchi hizo.
Akiwa ziarani
nchini China, Rais wa Sudan
Kusini, Salva Kiir, ameishutumu Sudan
kutangaza vita dhidi ya nchi yake.
Sudan imekanusha kufanya mashambulizi ya anga.
Mapigano ya hivi
karibuni ndio makubwa zaidi tangu Sudan Kusini kupata uhuru wake Julai mwaka
jana baada ya vita virefu na Sudan.