MARALIA ASILIMIA 50 YAYOKOMEZWA


MPANGO wa Taifa wa Kudhibiti Malaria (NMCP), umepunguza tatizo la malaria nchini kwa asilimia 50 ikiwa ni pamoja na vifo vya watoto walio chini ya umri wa miaka mitano.

Aidha, Mpango huo umeiomba Serikali zaidi ya Sh bilioni 5.1 kwa mwaka ujao wa fedha 2012/13 kwa ajili ya kupambana na ugonjwa wa malaria nchini.

Hayo ameyasema Meneja Mradi wa NMCP, Dk. Ally Mohammed wakati wa semina ya siku moja iliyoandaliwa na Taasisi ya Utafiti wa Magonjwa ya Ifakara, iliyofanyika Dar es Salaam.

Dk. Mohammed amesema fedha hizo ni katika kuongeza nguvu kutoka kwa misaada ya wahisani ambao wamekuwa mstari wa mbele kuisaidia nchini katika kupambana na ugonjwa huo.

Amesema Mpango wa Taifa wa Kudhibiti Malaria kwa muda wa miaka mitano kuanzia 2008 hadi 2013 na umekuwa na mafanikio ambapo ndani ya miaka mitatu, tatizo hilo limepungua asilimia 50 tangu mwaka 2008 hadi 2010.

Amesema licha ya kuwepo kwa mafanikio hayo, bado wanakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwamo na wananchi kutokuwa na matumizi sahihi ya vyandarua, kupata tiba sahihi na kutomaliza kiwango cha dawa walichopangiwa (dozi).

Dk. Mohammed amesema katika kupambana na tatizo hilo wamekuwa wakitumia mbinu mbalimbali kutokana na ukubwa wa tatizo na kuwa maeneo ambayo ni sugu wametumia mpango wa kupulizia dawa katika nyumba.