MITT Romney
ameshinda kura za maoni katika majimbo mengine matano, na kuimarisha nafasi
yake ya kuteuliwa kuwania uchaguzi wa rais wa Marekani hapo Novemba kwa tiketi
ya chama cha Republican.
Baada ya ushindi
katika majimbo hayo ya Connecticut, Rhodes Island, Delaware, New York na Pennsylvania,
Romney ameanza kuuangazia uchaguzi mkuu kwa kumlenga Rais Barack Obama na sera
zake za kiuchumi.
Akizungumza baada
ya ushindi huo, Romney amesema kampeni mpya imeanza sasa, na kumshambulia Rais
Obama, akisema muhula wake umekuwa wa ahadi za uongo na uongozi dhaifu.
Ikiwa inabakia
miezi sita kufanyika uchaguzi wa rais nchini Marekani, utafiti unaonyesha kuwa
hali ya uchumi ndio itakuwa suala muhimu katika uchaguzi huo.
Kura za maoni zinaonyesha kukaribiana kwa uungwaji mkono
kati ya Rais Obama na Mitt Romney, huku Obama akipewa nafasi ya kumpita
mpinzani wake kwa kura chache.