Majaji katika mahakama maalum kuhusu vita nchini Sierra Leone,
leo watatoa hukumu dhidi ya aliyekuwa Rais wa Liberia Charles Taylor kwa
kuhusika na vita hivyo vilivyodumu miaka 10.
Taylor
anasema kesi hiyo ni njama ya kisiasa
Taylor anakabiliwa na
mashtaka 11 ikiwemo ubakaji na mauaji ya raia wa Sierra Leone.
Ikiwa atapatikana na hatia atakuwa rais mstaafu wa kwanza
kuhukumiwa na mahakama ya kimataifa.
Kiongozi huyo wa zamani anadaiwa kufadhili waasi wa RUF.
Zaidi ya mashaidi 100 wamefika mbele ya mahakama hiyo lakini
Bw Taylor amekanusha kuhusika na uhalifu huo wakivita na anadai kuwa kesi hiyo
ni njama ya kummaliza kisiasa.
Hukumu ya majaji hao inasubiriwa kwa hamu sana
na raia nchini Sierra Leone
ambao jamaa zao waliathirika sana
wakati wa vita hivyo.
Inakadiriwa kuwa zaidi wa watu elfu 50 waliuawa na wengine
wakiwemo wanawake na watoto walibakwa na kukatwa mikono au miguu na waasi wa
RUF ambao upande wa mashtaka unasema walipata usaidizi wa silaha kutoka kwa Bw
Taylor.
Wakati wa vita hivyo, mwendesha mashtaka anasema kuwa Taylor alikuwa kiungo muhimu katika biashara haramu ya
almasi kutoka Sierra Leone.
Kesi hii iliodumu miaka mitatu na nusu, hata hivyo huenda
isi kamilike leo kwani pande zote wanauhuru wa kukata rufaa ikiwa hukumu hiyo
haitawaridhisha.