Rais wa zamani nchini Malawi, Bingu wa Mutharika,
amezikwa nyumbani kwake kusini mwa nchi. Wa Mutharika alifariki dunia
mwezi jana baada ya kupatwa na mshutuko wa moyo.
Bingu wa Mutharika alijenga makaazi yake mwaka 2004 pamoja na kaburi hilo ambalo alitaka kupumzishwa pamoja na mkewe aliyefariki dunia mwaka 2007 baada ya kuugua maradhi ya saratani.
Mwaka 2010 alimuoa Callista Chapola-Chimombo ambaye zamani alikuwa Waziri wa Utalii. Kakake rais, Peter Mutharika aliteuliwa na Bingu mrithi wake baada ya kustaafu mwaka ujao.
Baada ya kifo cha rais huyo kulikuwa na hofu kwamba wandani wake watajaribu kupuuza utaratibu wa katiba katika kupokezana madaraka kwa Joyce Banda ambaye alitofautiana na marehemu akiwa Makamu wake.
Bingu wa Mutharika ni mwanauchumi ambapo alisifiwa sana kutokana na sera zake kuimarisha sekta ya kilimo nchini Malawi. Hata hivyo mafanikio haya yalighubikwa lalama zilizoanza kumuandama rais huyo.
Alikosolewa vikali na wanaharakati wa kudhibiti uhuru wa vyombo vya habari, kukandamiza wapinzani wake wa kisiasa pamoja na usimamizi mbaya wa uchumi.