PAKISTAN: WAJANE WATATU NA WATOTO WA OSAMA WAHAMISHIWA SAUDI ARABIA
Maafisa wa serikali nchini Pakistan wanasema familia ya Osama Bin Laden, wajane wake watatu na watoto wao wamehamishiwa nchini Saudi Arabia mapema hii leo, takriban mwaka mmoja baada ya kiongozi huyo wa Al Qaida kuuliwa na vikosi vya Marekani.
Wajane hao na watoto wa Bin Laden walikuwa wakishikiliwa na maafisa wa Pakistan tangu alipouliwa Mei pili mwaka jana.
Baada ya miezi kumi kizuwizini, wajane na mabinti wawili wakubwa wa Bin Laden walihukumiwa na korti moja ya Pakistan kifungo cha siku 45 jela kwa makosa ya kuingia na kuishi kinyume na sheria nchini humo.
Kifungo chao kimemalizika tangu Jumanne iliyopita lakini mipango ya kuwarejesha Saudi Arabia iliakhirishwa kufuatia ripoti kuwa serikali ya Saudi Arabia ilikuwa haitaki wahamie nchini humo.