KWA HELI KANUMBA : MAMIA WAMIMINIKA MSIBANI


  •  MSIBA WAVUNJA REKODI YA KUKUSANYA WATU 
 
  • MAMIA WAZIMIA 
 
  • MAELFU WAKOSA NAFASI KA KUUAGA MWILI 
 
  • WALIOTOKA MOROGOGO WALALAMIKA


STIVINE KANUMBA ENZI ZA UHAI WAKE

JIJI la Dar es Salaam jana lilizizima kwa saa kadhaa kutokana na shughuli muhimu ya kutoa heshima za mwisho kwa aliyekuwa msanii maarufu wa tasnia ya filamu nchini, Steven Kanumba aliyefariki dunia mwishoni mwa wiki iliyopita.

Viwanja vya Klabu ya Viongozi (Leaders Club) wilayani Kinondoni, ndiko maelfu ya wakazi wa Jiji na mikoa jirani na wengine kutoka nje ya nchi walikofurika kumwona kwa mara ya mwisho na kumuaga kipenzi chao Kanumba.


Sambamba na Leaders baadhi ya barabara za wilaya hiyo zilifungwa kwa muda kuruhusu mwili wa marehemu Kanumba ‘The Great’ upitishwe ukitolewa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili hadi viwanjani hapo.


Kwa mujibu wa Kamati ya Mazishi, viti 10,000 viliandaliwa kwa ajili ya ugeni katika viwanja hivyo, lakini hadi saa 2 asubuhi vyote vilikuwa vimejaa na wengine kulazimika kusimama, huku baadhi wakipanda kwenye miti na magari ili kushuhudia kilichokuwa kikiendelea.


Viongozi waliohudhuria Heshima za mwisho ziliongozwa na Makamu wa Rais, Dk. Mohammed Gharib Bilal aliyefuatana na mkewe, Zakia Bilal na mke wa Rais, Mama Salma Kikwete wakiwamo pia viongozi mbalimbali na wasanii maarufu wa ndani na nje ya nchi.


Viongozi wengine waliohudhuria na kutoonekana kutokana na umati huo wa waombolezaji, alikuwa Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Dk. Emmanuel Nchimbi, na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka.


Wengine ni Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Meck Sadik. Pia walikuwapo mameya wa Dar es Salaam, Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Jordan Rugimbana na baadhi ya wabunge; wa Kinondoni, Idd Azzan; wa Ubungo, John Mnyika na wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi ‘Mr Sugu’.


Mwili wa marehemu uliingizwa uwanjani saa 4 asubuhi na kufuatiwa na mama wa marehemu, Flora Mtegoa na watoto walioigiza na marehemu Kanumba, Jamila na Jalia Jeilani. Kuwasili kwa watoto hao kulisababisha dada wa Kanumba, Adela kuzimia.


Mbali na dada huyo walikuwapo baadhi ya wasanii na wananchi waliokuwa wakianguka na kupoteza fahamu ambapo walikuwa wakipatiwa huduma ya kwanza. Mwili huo ulipofikishwa uwanjani ulibebwa na wasanii na kuwekwa katika jukwaa maalumu lililokuwa limeandaliwa na msanii Steve Nyerere ndiye aliyekuwa amebeba msalaba.


Akitoa mahubiri katika viwanja hivyo, Mchungaji Daud Samweli wa Kanisa la African Inland Church la Chang’ombe, aliwataka wananchi kujiandaa wakati wote na kufanya mambo mema ili wanapokufa waache kitu nyuma kitakachokumbukwa na jamii.


“Inatupasa sote tuwe na kitu tutakachokiacha nyuma ili tukifa kiendelee kuzungumzwa …Kanumba ameacha kitu kwetu kitakachoendelea kuishi kutokana na kazi zake ambazo amekuwa akizifanya,” alisema.


Alisema kuna watu wanakufa, lakini hawaachi kumbukumbu yoyote nyuma, lakini Kanumba ameacha kitu hivyo ni wajibu wa kila mmoja kumuenzi.


Akitoa salamu za Serikali, Dk. Nchimbi alisema Serikali imepokea kwa masikitiko makubwa msiba huo na mamilioni ya watu wanaufuatilia na kumlilia Kanumba si kwa vile alikuwa Rais au Mbunge, bali ni kutokana na uhusiano wake na jamii. Alisema Serikali imetoa ubani wa Sh milioni 10.


Rais wa Shirikisho la Filamu Tanzania, Simon Mwakifwamba alisema wamepoteza komando na uwezo wake wanautambua kwa kuwa amekuwa akiitangaza Tanzania vizuri nje ya nchi. Wananchi wavamia jukwaa Wananchi ambao kutokana na msongamano uliokuwepo walifikia hatua ya kuvamia jukwaa lililokuwa limekaa wageni waalikwa wakiwemo mawaziri ambao walilazimika kuondoka na kuwapisha.


Katika maombolezo hayo, baadhi ya wananchi walionekana kutoridhika na kitendo cha mabadiliko ya ratiba, ambapo walioruhusiwa kuuaga mwili kwa kuuangalia katika jeneza, walikuwa viongozi na ndugu wa karibu. Katika taarifa za awali wananchi waliambiwa kuwa ratiba ya kuuaga ingeanza saa 6 mchana baada ya misa hadi saa 9 alaziri na maziko kuwa saa 10 jioni, lakini badala yake utaratibu wa kuaga uliishia saa 5.45 na mwili kuondolewa na kuelekea katika makaburi ya Kinondoni.


Wananchi hao ambao walihamasishwa na vyombo vya habari kujitokeza kwa wingi, walilalamika kuwa kitendo walichofanyiwa cha kujipanga barabarani na kuangalia jeneza likipita si cha kiungwana, kwa kuwa walichokuwa wakihitaji ni kupita mmoja mmoja kuuaga mwili wa marehemu.


Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari jana, Mnyika alisema aliahirisha safari yake ya bungeni ili ashiriki kutoa heshima za mwisho. Hata hivyo, alisema yeye alikuwa miongoni mwa viongozi waliokosa nafasi ya kuaga mwili wa Kanumba, ambaye alikuwa mkazi wa jimbo analoliongoza, kutokana na wingi wa watu.


Alisema Kanumba alipenda mabadiliko katika maisha yake na Taifa lake na kuongeza kuwa filamu zake zitaacha kumbukumbu ya kudumu katika jamii.


Hata hivyo, wakati gari lililobeba mwili huo likitoka, wananchi walilizingira na kuimba “Mshushe tumbebe!” Kelele ambazo hazikuzaa matunda, kwani walikuwapo askari waliosimamia na kulinda usalama wa taratibu zote za mazishi. Aidha, wananchi walilalamika kuwa eneo hilo halikuwa salama kwa kuwa walishindwa kudhibiti watu na kupendekeza panapotokea tukio lingine kama hilo, lipangwe eneo kubwa kama Uwanja wa Taifa ili kila anayeingia kutoa heshima zake ashuhudie kila kinachoendelea.


Umati wa wananchi wengi wakiwa wa kawaida kutoka Mkoa wa Morogoro ambao walishushwa na mabasi matatu ya Abood, wengine kutoka Pwani na pembe za Jiji la Dar es Salaam, ulitanda barabarani na kusababisha msafara wa msanii huyo kuchukua zaidi ya saa mbili kutoka viwanja vya Leaders hadi makaburi ya Kinondoni.


Mama Kanumba ashindwa kuzika Katika maziko, mama mzazi wa Kanumba, Flora alilazimika kuondoka makaburini hapo baada ya kushindwa kuvumilia kushuhudia mwili wa mwanawe ukiwekwa kaburini. Kutokana na hali hiyo mashada ya maua ya familia yaliwekwa na watu mbalimbali akiwamo dada wa marehemu, Adela na Mbunge wa Maswa Magharibi, John Shibuda (Chadema) aliyemwakilisha baba mzazi, Charles Kanumba.


Shughuli za maziko zilifanyika na kuchukua takribani saa tatu, ikiwa chini ya ulinzi mkali, kukiwa na magari ya Polisi, gari ya maji ya kuwasha kikosi cha mbwa na kile cha farasi, lakini eneo la makaburi watu walijaa kupita kiasi nje na ndani ya uzio wa makaburi huku wengine wakiwa wamepanda juu ya miti kutaka kushuhudia tukio hilo. Wang’ang’ania kuona kaburi Saa 9.40 baada ya kumaliza shughuli za mazishi hali ilibadilika makaburini hapo baada ya umati wa wananchi uliokuwa ndani na ule uliokuwa nje kutaka kubaki kushuhudia kaburi la nyota huyo baada ya kukosa nafasi ya kuaga. Pamoja na gari la Polisi namba PT 0890 kuwataka wananchi wote kuondoka eneo hilo kwa amani kutokana na shughuli za mazishi kukamilika, hawakutii mpaka ilipofika saa 10.30 jioni ambapo polisi walilazimika kutumia mbinu nyingine ya kuwaondoa wananchi hao. Ndani ya dakika 15, Polisi waliokuwa kwenye magari, na wale waliokuwa chini walifanikiwa kuwaondoa watu wote ndani ya makaburi hayo na kutoa amri watu wote waliosimama nje ya barabara kwenda makwao na kupisha barabara ili magari yapite. Watu 600 chali Aidha, katika maziko hayo, watu zaidi ya 600 walidondoka na kupoteza fahamu wakiwamo waigizaji Wema Sepetu na Irene Uwoya ambaye hali ilikuwa mbaya akakimbizwa hospitalini na gari la wagonjwa. Kiongozi wa kikosi cha Huduma ya Kwanza ya Msalaba Mwekundu, Dk. Nassor Matuzya alisema watu wengine walipatiwa matibabu katika eneo maalumu walilolitenga. “Zaidi ya watu 600 walidondoka na tumewahudumia na wako katika hali nzuri, na watu watatu tu ndio ambao tumelazimika kuwapeleka Hospitali ya Mwananyamala na taarifa nilizonazo mpaka sasa wanaendelea vizuri,” alisema Dk. Matuzya. Madaktari Sinza, Mwananyamala Jopo la madaktari na watoa huduma walitoka katika Hospitali ya Sinza, Hospitali ya Mwananyamala, Taasisi ya Bima ya Ndege Medical, Chama cha Msalaba Mwekundu na Shirika la Kimataifa la Kuhudumia Wakimbizi (UHNCR). Wasanii wageuka kivutio Aidha, katika maziko hayo, wananchi wengi walikuwa wakivutiwa na wasanii mbalimbali walioko msibani hapo huku wengine wakitaka hata wawaguse au kuwakumbatia na kuonesha kufurahi kuonana nao ana kwa ana. Wajasiriamali wanufaika Wajasiriamali wadogo walitekeleza usemi wa ‘kufa kufaana’, baada ya kutumia wingi wa watu waliojitokeza kumuaga Kanumba, kuwa fursa kwao ya kibiashara. Wakizungumza na gazeti hili kwa nyakati tofauti baadhi ya wajasiriamali hao walieleza kuwa mkusanyiko wa watu waliojitokeza katika mazishi, uliwapa wateja wengi walionunua bidhaa zao hususan vinywaji.


Katika baa ya GL iliyopo Sinza Vatican ambako kulikuwa na maombolezo ya siku tatu, mama lishe Mama Adam, aliliambia gazeti hili kuwa kwa siku hizo tatu, aliuza chakula kingi kuliko alivyotarajia. Alisema wateja wengi walikuwa wanatoka msibani ambapo licha ya kununua vinywaji katika baa GL pia walinunua mishikaki, wali na bidhaa nyingine muhimu kwake.


Hali hiyo pia ilikuwa katika baa jirani ya Tea Garden ambako nako muda wote ilionekana kujaa watu wengi waliokuwa wakila na kunywa. Fundi cherehani Gazeti hili lilishuhudia siku moja kabla ya msiba, nguo aina ya fulana na dera zenye picha ya Kanumba zikiuzwa kwa wingi katika msiba huo ambapo dera moja liliuzwa kwa Sh 30,000 huku fulana ikiuzwa Sh 10,000. Fundi cherehani wa eneo jirani ya nyumba ya msanii huyo hadi saa nane usiku wa kuamkia jana alikuwa akishona dera hizo hali iliyoashiria kuwa hata yeye alipata wateja wengi.


Muuza duka Katika Viwanja vya Leaders biashara ilikuwa nzuri kwa wajasiriamali ambapo gazeti hili lilimnukuu Juma Ali ambaye ni muuza duka jirani na viwanja hivyo, akisema alinunua soda nyingi na katoni za maji lakini zilikwisha na kurudia kununua mara tatu. Daladala nauli juu Pia katika eneo la Mwenge kulikuwa na mabasi ambayo yalikuwa yakitoza hadi Sh 500 ikiwa ni nauli ya kutoka eneo hilo kwenda Leaders ambapo mabasi hayo yalijaa watu. Imeandikwa na Anastazia Anyimike, Hellen Mlacky na Evance Ng’ingo.